Serikali ya Slovenia yaidhinisha hoja ya kuitambua nchi huru ya Palestina
(last modified Fri, 31 May 2024 09:58:26 GMT )
May 31, 2024 09:58 UTC
  • Serikali ya Slovenia yaidhinisha hoja ya kuitambua nchi huru ya Palestina

Vyombo vya habari vya Slovenia vimetangaza kuwa serikali ya nchi hiyo imeidhinisha hoja ya kuitambua Palestina kuwa ni nchi rasmi na huru.

Waziri Mkuu Robert Golob alisema baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kwamba Serikali imepeleka hoja hiyo kwenye Bunge la Taifa ili kuidhinishwa rasmi. Bunge la Taifa la Slovenia linatarajiwa kupigia kura hoja hiyo wiki ijayo.
 
Wizara ya Mambo ya Nje ya Slovenia imeeleza kuwa mchakato wa kuitambua Palestina huru "unatuma ishara kali kwa nchi nyingine" kuiga mfano wa Slovenia, Ireland, Norway na Uhispania.
 
Wizara hiyo imebainisha kuwa kutambuliwa kwa Palestina kunathibitisha tena jukumu la Slovenia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama "mtetezi wa amani na usalama" na msimamo wa muda mrefu wa nchi hiyo kwamba "suluhisho la kudumu la mzozo wa Mashariki ya Kati linaweza kupatikana tu kwa kuundwa mataifa mawili".

Hatua hiyo ya serikali ya Slovenia ambayo ilitangazwa jana Alkhamisi, imechukuliwa baada ya kupita siku mbili tu tangu Ireland, Norway na Uhispania zilipotangaza rasmi kuitambua nchi huru ya Palestina.

 
Mnamo Mei 9, serikali ya Slovenia ilizindua mchakato wa kuitambua nchi huru ya Palestina.
 
Hivi karibuni, Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya alisema nchi nne wanachama wa EU ambazo ni Uhispania, Ireland, Slovenia, na Malta zipo mbioni kulitambua taifa huru la Palestina na akadokeza kuwa, yumkini Ubelgiji na nchi nchi nyingine kadhaa za Ulaya zikafuata msimamo huo wa kuitambua nchi huru ya Palestina.

Harakati hizo za kulitambua taifa huru la Palestina zinaendelea katika hali ambayo, azimio lililopendekezwa na nchi za Kiarabu kuhusu uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa liliidhinishwa kwa wingi wa kura mnamo tarehe 10 Mei katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.../