Jul 27, 2024 10:17 UTC
  • Thuluthi moja ya nchi zote duniani zimewekewa vikwazo na Marekani

Gazeti la Marekani la Washington Post limetoa ripoti inayoonyesha kuwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, serikali ya nchi hiyo imeweka vikwazo vya kiuchumi na visivyo na athari yoyote dhidi ya thuluthi moja ya nchi zote duniani.

Washington Post limeeleza katika ripoti yake hiyo ya uchambuzi kwamba, serikali moja baada ya nyingine za Marekani kuanzia miaka ya 1990 zimegeuza vita vya kiuchumi na kuweka vikwazo vya kiuchumi kuwa nyenzo kuu za sera zao za nje, lakini sehemu kubwa ya vikwazo hivyo havijawa na taathira na vimekuwa na athari kinyume na ilivyokusudiwa.
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vikwazo ilivyowekewa Korea Kaskazini kwa miongo kadhaa vimeshindwa kuzuia mipango ya silaha ya Pyongyang.
 
Ripoti ya Washington Post imeendelea kueleza kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Nicaragua na Cuba pia havikuwa na taathira yoyote ya kuwezesha kuzipindua serikali za nchi hizo.
 
Kwa mujibu wa Washington Post, kiwango cha vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi mbalimbali duniani ni kikubwa zaidi mara tatu kulinganisha na nchi au taasisi yoyote ya kimataifa.

Wakati huo huo, Matthew Miller, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, alitangaza katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa kwamba nchi hiyo itaendelea kutekeleza vikwazo vyake vyote dhidi ya Iran.

Washington imeweka vikwazo zaidi ya 600 na vizuizi vya kusafirisha bidhaa nje dhidi ya Iran kwa visingizio na madai hewa na ya uwongo.
 
Kati ya Februari 2022 hadi Januari 2024, Marekani imewawekea vikwazo zaidi ya watu 16,000, makampuni elfu tisa na asasi 3,200 zenye uhusiano na Russia, kikiwa ni kiwango cha juu zaidi cha vikwazo kuwekwa duniani kote.../

 

Tags