Machafuko yanaendelea nchini Uingereza
Miji kadhaa ya Uingereza imekuwa uwanja wa ghasia za mitaani na makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa makundi ya mrengo wa kulia na vile vile wapinzani na watu wenye chuki dhidi ya wahajiri wa Kiiislamu.
Shirika la habari la IRIB limeripoti kuwa ghasia hizo zilizuka baada ya kusambazwa taarifa za uongo kuhusu tukio la kudungwa kisu mtu mmoja kwenye hafla katika mji wa Southport kaskazini magharibi mwa Uingereza.
Shambulio hilo la kisu lilitokea siku ya Jumatatu tarehe 29 Julai, katika mji wa Southport na kuzua wimbi la chuki dhidi ya Uislamu kote Uingereza ambapo athari zake bado zinaendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo na miji ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na Manchester, Southport, Sunderland, Maryside, Bristol, Nottingham, Belfast na Liverpool.
Polisi ya Uingereza imetangaza kuwa idadi kadhaa ya misikiti na makazi ya wahajiri wa Kiislamu yameshambuliwa katika mji wa Southport. Katika shambulio hilo wasichana watatu wadogo wameuawa kwa kuchomwa visu na vile vile watu 10 wakiwemo watoto wanane wamejeruhiwa.
Mshukiwa wa shambulio hilo kwa madai ya uwongo ya mitandao ya kijamii ya mrengo wa kulia, ni kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 17 na ambaye ni mtafuta hifadhi ambaye aliingia Uingereza kwa boti, huku polisi wakisema katika taarifa kuwa mshukiwa huyo ni mzaliwa wa Uingereza.
Aidha polisi wanasema wamewaweka karibu askari elfu nne katika hali ya tahadhari ili kurejesha utulivu nchini. Wanasema makumi ya polisi wamejeruhiwa baada ya kupigwa mawe, fimbo, mada za moto, matofali, chupa na vifaa vya kuzimia moto na pia kwamba makumi ya watu wamekamatwa katika matukio hayo.
Polisi wa Uingereza wanaamini kwamba kundi la "British Defense League" ambalo ni kundi lenye itikadi kali na misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu ndilo limeandaa ghasia zinazoendelea huko Southport kaskazini magharibi mwa Uingereza.
Wakati huo huo, kundi la kupinga ubaguzi wa rangi la "Hope Not Hate" limetangaza kuwa ghasia nyingine 30 zimepangwa kufanyika wiki hii nchini humo.