Aug 09, 2024 10:09 UTC
  • Muhammad Yunus ala kiapo cha kuongoza serikali ya mpito ya Bangladesh

Mwanauchumi aliyeshinda tuzo ya amani ya Nobel Muhammad Yunus ameapishwa kuwa mkuu wa serikali ya mpito ya Bangladesh, siku tatu baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kulazimika kujiuzulu na kukimbilia nchi jirani ya India.

Yunus, mwenye umri wa miaka 84, alikula kiapo katika hafla iliyofanyika kwenye ikulu ya rais mjini Dhaka Alkhamisi usiku ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa kisiasa, wakuu wa mashirika ya kiraia, majenerali na wanadiplomasia.
 
"Nitazingatia, kuunga mkono na kulinda katiba," Yunus alisema alipoapishwa na Rais Mohammed Shahabuddin, akiongeza kwamba atafanya kazi zake "kwa uaminifu".

Zaidi ya wajumbe kumi wa baraza lake la mawaziri, ambao vyeo vyao ni washauri, na si mawaziri, pia walikula kiapo, ambapo serikali yake ya muda itakuwa na jukumu la kurejesha amani na kujiandaa kwa uchaguzi mpya.

Hao ni pamoja na Nahid Islam na Asif Mahmud, viongozi wakuu wa kundi la Wanafunzi wa Kupinga Ubaguzi, ambalo liliongoza maandamano ya wiki moja ambayo yalimuondoa Hasina.

Wengine ni pamoja na Touhid Hossain, katibu wa zamani wa mambo ya nje, na Hassan Ariff, mwanasheria mkuu wa zamani. Syeda Rizwana Hasan, mwanasheria wa mazingira aliyeshinda tuzo, na Asif Nazrul, profesa mkuu wa sheria na mwandishi, nao pia waliapishwa.

Sheikh Hasina

Adilur Rahman Khan, mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na serikali ya Hasina, pia alikula kiapo kama mshauri.

Hakukuwa na mwakilishi yeyote kutoka chama cha Awami League cha Hasina aliyehudhuria hafla hiyo.

Sheikh Hasina alijiuzulu siku ya Jumatatu baada ya maandamano ya nchi nzima yaliyoanza mwezi Julai kupinga mfumo wa upendeleo wa nafasi za kazi serikalini ambao wakosoaji walisema unapendelea watu wenye uhusiano na chama chake.

Hata hivyo maandamano ya hivi karibuni yalikuwa changamoto kubwa kwa utawala wa miaka 15 wa Hasina kwa sababu zaidi ya watu 300, wakiwemo wanafunzi, waliuawa wakati wa ghasia hizo.../

Tags