Hakuna mtu aliyenusurika katika ajali ya ndege Brazil
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115060-hakuna_mtu_aliyenusurika_katika_ajali_ya_ndege_brazil
Watu 61 wameaga dunia baada ya ndege ya abiria iliyokuwa imewabeba kuanguka nchini Brazil.
(last modified 2025-10-18T05:48:37+00:00 )
Aug 10, 2024 11:11 UTC
  • Hakuna mtu aliyenusurika katika ajali ya ndege Brazil

Watu 61 wameaga dunia baada ya ndege ya abiria iliyokuwa imewabeba kuanguka nchini Brazil.

Ndege hiyo ya Kampuni ya VoePass iliyokuwa imebeba abiria 57 na wahudumu wanne imeanguka huko São Paulo, kusini mashariki mwa Brazil na kupelekea vifo vya watu wote 61 waliokwemo kwenye ndege hiyo aina ya ATR 72-500.

Shirika la habari la Mehr limeandika habari hiyo na kuongeza kuwa, ndege hiyo iliondoka Cascavel katika jimbo la Parana nchini Brazil ikielekea São Paulo, ambapo ilipoteza mawasiliano ikiwa angani na kuanguka kwenye makazi ya watu na kisha kuripuka.

Shirika la VoePass limesema katika taarifa kuwa, “Kampuni inasikitika kuufahamisha umma kwamba watu wote 61 waliokuwa kwenye ndege nambari 2283 wamekufa katika eneo la tukio."

Mamlaka zimesema pamoja na kwamba ndege hiyo ilianguka kwenye makazi ya watu, hakuna yeyote aliyejeruhiwa au kufariki kati yao, na kwamba waliofariki ni abiria wote waliokuwemo kwenye ndege pekee.

Gavana wa São Paulo, Tarcísio Gomes de Freitas ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia ajali hiyo. Hii ni ajali mbaya zaidi katika historia ya ajali za ndege nchini Brazil, tangu ajali ya 2009 ya ndege kutoka Rio de Janeiro kwenda Paris ambayo ilitumbukia katika Bahari ya Atlantiki, na kuua watu wote 228.