China: Marekani ndio tishio kubwa zaidi la nyuklia duniani
Aug 17, 2024 10:27 UTC
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China amesema, Marekani ndiyo hatari kubwa zaidi kwa dunia endapo yatatokea mapigano ya nyuklia.
Beijing imewashutumu maafisa wa Washington kwa kuchukua maamuzi yasiyo ya uwajibikaji kwa lengo la kudumisha ubeberu wake, hasa kwa kutoa vitisho kwa jamii ya kimataifa kwa maghala yake ya silaha za nyuklia.
Matamshi hayo yametolewa na Zhang Xiaogang, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China, akijibu uamuzi wa Pentagon wa kuvizatiti vikosi vya Marekani vilivyoko nchini Japan.
Katika mkutano aliofanya hivi majuzi na maafisa wa Japan, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin aliyaelezea mabadiliko hayo kama "moja ya mabadiliko imara zaidi katika uhusiano wa kijeshi kati ya Tokyo na Washington katika miaka 70 iliyopita."
Katika mkutano huo, Marekani iliahidi kuilinda Japan kwa nguvu na uwezo wake wote, ikiwemo kutumia uwezo wake wa nyuklia.
Katika mjibizo aliotoa kwa mkutano huo, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China amesema: hatua kama hizo zitazusha makabiliano tu na kudhoofisha uthabiti na amani ya kikanda.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Wizara ya Ulinzi ya China, Marekani ndiyo tishio kubwa zaidi la nyuklia duniani kwa sababu ina maghala makubwa zaidi ya silaha za nyuklia na inatekeleza sera inayoipa ruhusa nchi hiyo ya kutangulia kutumia silaha hizo kabla ya kushambuliwa.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China amesisitiza kwa kusema: "hatua za hivi karibuni za Marekani nchini Japan zitazidisha mivutano tu na kuongeza hatari ya kuenea silaha na makabiliano ya nyuklia ya kikanda".../