Watu watatu, wengine wajeruhiwa vibaya katika shambulizi la kisu Ujerumani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115576-watu_watatu_wengine_wajeruhiwa_vibaya_katika_shambulizi_la_kisu_ujerumani
Watu watatu wameuawa na wanne kujeruhiwa vibaya katika shambulizi la kisu lililotokea wakati wa tamasha katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Solingen Ijumaa usiku huku uhalifu ukiongozeka katika nchi hiyo ya Ulaya.
(last modified 2024-08-24T03:07:39+00:00 )
Aug 24, 2024 03:07 UTC
  • Watu watatu, wengine wajeruhiwa vibaya katika shambulizi la kisu Ujerumani

Watu watatu wameuawa na wanne kujeruhiwa vibaya katika shambulizi la kisu lililotokea wakati wa tamasha katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Solingen Ijumaa usiku huku uhalifu ukiongozeka katika nchi hiyo ya Ulaya.

Msemaji wa polisi ya mji ulio karibu wa Dusseldorf amesema polisi imeanzisha operesheni kubwa ya kumsaka mtu anayeshukiwa kutekeleza jinai hiyo. Mshambuliaji huyo aliwashambulia watu kiholela akitumia kisu.

Tamasha hilo lilikuwa sehemu ya mfululizo wa matukio ya kusherehekea miaka 650 ya kuanzishwa mji huo. Watu walikusanyika mjini humo Ijumaa jioni katika siku ya kwanza ya tamasha la siku tatu la kusherehekea kuasisiwa kwake. Zaidi ya wageni 75,000 walitarajiwa kuhudhuria sherehe hizo za siku tatu ambazo sasa zimefutwa.

Ujerumani imeshuhudia mfululizo wa mashambulizi ya visu katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, huku Waziri wa Mambo ya Ndani Nancy Faeser akiahidi kukabiliana na uhalifu wa kutumia visu.

Afisa wa polisi aliuawa na watu watano kujeruhiwa katika shambulio la kisu kwenye mkutano wa mrengo wa kulia katika mji wa Mannheim mwishoni mwa mwezi Mei.

Ujerumani ilirekodi ongezeko kubwa la uhalifu wa kutumia nguvu mnamo 2023.

Mwezi Machi gazeti la Welt am Sonntag lilichapisha ripoti maalumu iliyosema uhalifu mwaka jana ulipanda kwa asilimia 8.6, ikiwa ni ongezeko la juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 15.