Mkutano wa wanadiplomasia wakuu wa Afrika mjini Tokyo umeendelea leo Jumapili
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115626-mkutano_wa_wanadiplomasia_wakuu_wa_afrika_mjini_tokyo_umeendelea_leo_jumapili
Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo unaowakusanya pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje kwa ajili ya kujadiliana Maendeleo ya Afrika (TICAD) ambao ulifunguliwa jana Jumamosi umeendelea leo Jumapili katika mji mkuu wa Japan, Tokyo.
(last modified 2024-08-25T06:57:25+00:00 )
Aug 25, 2024 06:57 UTC
  • Mkutano wa wanadiplomasia wakuu wa Afrika mjini Tokyo umeendelea leo Jumapili

Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo unaowakusanya pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje kwa ajili ya kujadiliana Maendeleo ya Afrika (TICAD) ambao ulifunguliwa jana Jumamosi umeendelea leo Jumapili katika mji mkuu wa Japan, Tokyo.

Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na wanadiplomasia wakuu na maafisa wengine wakuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan anayehusika na masuala ya Bunge, Yoichi Fukazawa amesema kuwa, imebaki miaka mitano tu kufikia mwaka 2030, tarehe iliyopangwa kufikia malengo ya kuweko huduma za afya kwa wote, lengo ambalo Japan imejitolea kulifanikisha na kuongoza juhudi za kimataifa kuhakikisha lengo hilo linafikiwa barani Afrika.

Tokyo, mji mkuu wa Japan

 

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan, Fukazawa pia amesema: "Jumuiya ya kimataifa lazima ijikumbushe tena wajibu wa kufanikishwa makusudio ya UHC na ichukue hatua kabla ya kusahauliwa uzoefu mchungu na somo tulilojifunza kutokana na janga la UVIKO-19." 

Pia amesisitizia haja ya kubadilishana ujuzi na kukuza ushirikiano ili kuhakikisha kuna upatikanaji sawa na wa pamoja wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na chanjo kwa wote.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Japan, lengo la mkutano huo ni kufanya majadiliano kuhusu mkutano wa "TICAD 9" wa mwaka ujao ambao umepangwa kufanyika mwezi Agosti mwakani katika jiji la bandari la Yokohama huko Japan.