Mgogoro wa kisiasa nchini Ufaransa na hali ngumu inayomkabili Macron
Mamia ya watu wa Ufaransa wameandamana katika mitaa ya Paris na kukusanyika katika uwanja wa Danfer-Rochereau, wakipiga nara dhidi ya Rais Emmanuel Macron na kumtaka ajiuzulu mora moja.
Wakati wa maandamano hayo ambayo yalifanyika mjini Paris kwa wito wa Chama cha Wazalendo, waandamanaji walipga nara kama vile "Macron jiuzulu!", "Macron toka nje" na "Macron, umekwisha", wakimtaka aondoke katika Ikulu ya Elysee mara moja.
Nara zinazopigwa dhidi ya Macron, ambaye nchi yake inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa, inaelezea wazi kuongezeka hasira za Wafaransa na upinzani wao dhidi ya utendaji wake. Hii ni kwa sababu Ufaransa imeshindwa kuunda serikali hata baada ya kufanyika uchaguzi wa bunge wa mapema siku 45 zilizopita, suala ambalo linakosolewa vikali na wananchi wa Ufaransa. Karibuni hivi, Macron pia alipinga kuundwa serikali ya mrengo wa kushoto.
Hossein Mousavi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema kuhusu suala hili: "Huenda Macron hakudhani kwamba Ufaransa ingekabiliwa na mgogoro wa kisiasa wa hivi sasa baada ya kuamua kuvunja bunge na kuandaa uchaguzi wa mapema. Lakini mchakato wa kisiasa na ushindi wa watu wenye itikadi kali, hasa katika duru ya kwanza ya uchaguzi, umemfanya Macron na hata Ufaransa kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa ambapo sasa rais huyo anatakiwa ajiuzulu mara moja."
Washiriki wa maandamano hayo dhidi ya Macron walibeba mabango na maberamu yaliyoandikwa maandishi yaliyosomeka "demokrasia yetu imedhoofika", "kila kitu kimeharibiwa", "tunapinga udikteta" na "Macron lazima ukomeshwe." Kauli mbiu kama hizo dhidi ya rais wa Wafaransa zinaonyesha wazi kuwa nchi hiyo imeingia kwenye mzozo wa kisiasa ambao unaweza kumwangusha hata Macron mwenyewe, haswa ukitiliwa maanani kuwa rais huyo anatuhumiwa kukiuka katiba ya nchi.
Mmoja wa washiriki wa maandamano hayo ameeleza kuwa Macron amekiuka Katiba ya Ufaransa na kutozingatia maoni ya wananchi. Amesisitiza kuwa saini za wabunge 58 zinatosha kuzindua mchakato wa kutekeleza Ibara ya 68 ya Katiba ya nchi na hivyo kutoa uwezekano wa kumfukuza kazi Rais Macron.
Kwa mujibu wa gazeti la Kiingereza la The Guardian, watu wa Ufaransa wanamchukulia Macron kuwa rais wa kiimla aliyeshindwa kutekeleza majukumu yake na ambaye umaarufu wake unaendelea kupungua kila siku. Wanasema, tabia kama hiyo haiwezi kukubalika katika mfumo wa demokrasia. Kwa msingi huo, wapiga kura wa Ufaransa wameonyesha wazi upinzani wao dhidi ya siasa za Macron, na wanamtaka aheshimu maoni yao.
Rais wa Ufaransa Jumatatu ya wiki iliyopita alipinga kuundwa kwa serikali ya mrengo wa kushoto kwa hoja kuwa serikali hiyo ni tishio kwa uthabiti wa taasisi za nchi. Ingawa muungano wa mrengo wa kushoto ulishinda viti vingi vya ubunge katika uchaguzi wa Julai, lakini haukuweza kupata wingi wa kura kwa ajili ya kuunda serikali. Kwa hivyo, inaonekana kwamba ucheleweshaji mambo na upinzani wa Macron kwa ajili ya kuundwa serikali mpya ya nchi hiyo kumewachosha Wafaransa ambao hawataki kumuona tena uongozini.