Venezuela yailaani Washington kwa kuiiba ndege yake, yaapa kulipiza kisasi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i115956-venezuela_yailaani_washington_kwa_kuiiba_ndege_yake_yaapa_kulipiza_kisasi
Serikali ya Venezuela jana Jumatatu iliilaani vikali Washington kwa kitendo chake cha kuiteka ndege ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na kukitaja kitendo hicho kuwa ni muendelezo wa uharamia na uhalifu wa Marekani.
(last modified 2024-09-03T03:17:16+00:00 )
Sep 03, 2024 03:17 UTC
  • Venezuela yailaani Washington kwa kuiiba ndege yake, yaapa kulipiza kisasi

Serikali ya Venezuela jana Jumatatu iliilaani vikali Washington kwa kitendo chake cha kuiteka ndege ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na kukitaja kitendo hicho kuwa ni muendelezo wa uharamia na uhalifu wa Marekani.

Marekani imeiteka ndege hiyo katika Jamhuri ya Dominica, ikidai kuwa eti upatikanaji wake umekwenda kinyume na vikwazo vya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Yvan Gil, amesema katika mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba, Venezuela inaishitakia jumuiya ya kimataifa kwamba kwa mara nyingine tena, Marekani imeendeleza uhalifu wake na imeonesha kuwa haijui kitu kingine isipokuwa uharamia.

Amesema: Marekani imeiba ndege ambayo imekuwa ikitumiwa na Rais wa nchi yetu kwa madai ya kukiukwa vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Venezuela na ambavyo ni kinyume cha sheria zote duniani."

Waziri Yvan Gil pia amesema: "Venezuela inatangaza wazi kuwa ni haki yake kuchukua hatua zozote za kisheria kukabiliana na uhalifu huo wa kiserikali pamoja na madhara yoyote yatakayosababishwa na uharamia huo wa Marekani. 

Mapema leo Jumanne, vyombo vya habari vimeripoti taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Mahakama ya Marekani ikitangaza kuwa, Washington imeteka ndege iliyokuwa inatumiwa na Rais Nicolas Maduro wa Venezuela katika ardhi ya Dominican, hatua ambayo Venezuela imesema ni uharamia wa kiserikali na imeapa kulipiza kisasi.