Mashia wauawa Afghanistan katika hujuma ya magaidi wa Daesh
Raia takribani 14 wameuawa katika shambulizi la kigaidi la kundi la Daesh nchini Afghanistan ambapo walikuwa wamekusanyika kuwakaribisha wafanyaziara wanaowasili kutoka maeneo matakatifu mjini Karbala, Iraq.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Afghanistan, shambulio hilo lilitokea Alhamisi saa sita mchana katika eneo la Karyudal, ambalo liko kwenye mpaka kati ya mikoa ya Daykundi na Ghor.
Ripoti zinaonyesha kuwa waliouawa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia kutoka wilaya ya Sang Takht katika mkoa wa Daykundi, ambao walikuwa wamesafiri hadi Karyudal kukutana na jamaa zao wa kabila laHazara waliokuwa wakirejea kutoka ziyara katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq.
Inasemekana wavamizi hao walisimamisha basi lililokuwa limewabeba wakazi hao kwa kisingizio cha kupiga picha na kisha kuwafyatulia risasi.
Katika taarifa jana jioni, magaidi wakufurishaji wa kundi la Daesh Khorasan walilidai kuhusika na shambulio hilo.
Wakati huo huo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amelaani shambulizi hilo la kigaidi katika taarifa yake ya Ijumaa ambapo pia ametoa salamu za rambirambi kwa familia za wahanga.
Amesema Iran inaunga mkono hatua za kukabiliana na ugaidi zinazochukuliwa na utawala wa Taliban nchini Afghanistan, huku akitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuwaadhibu wahusika wa jinai hiyo.
Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaunda kundi la wachache nchini Afghanistan ambao wengi wao wanatoka katika jamii ya Wahazara nchini humo.
Mashia ni takriban asilimia 22 ya watu wa Afghanistan na wamekuwa wakidhulumiwa na kulengwa katika matukio kadhaa makubwa ya utekaji nyara na mauaji. Magaidi wakufurishaji wa Daesh wamekuwa wakitekeleza mashambulizi dhidi ya Mashia kote Afghanistan.