Askari kadhaa walichinjwa hadharani Uturuki baada ya jaribio la mapinduzi
Duru za habari nchini Uturuki zimeripoti kwamba, askari waliojaribu kufanya mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli hivi karibuni nchini Uturuki, walikubwa na ukatili wa kutisha ikiwemo kuuawa, kuchinjwa au kukatwa viungo vyao vya mwili.
Hii ni katika hali ambayo serikali za mataifa kadhaa zilikuwa zimeitaka serikali ya Uturuki kujiepusha kufanya aina yoyote ya ukatili au umwagaji damu kutokana na ulipizaji kisasi dhidi ya askari waliohusika.
Kuhusiana na hilo, mtandao wa Middle East Online umeonyesha sehemu moja ya mkanda wa video ambao unaonyesha baadhi ya askari wakiwa wanachinjwa na askari watiifu kwa serikali usiku wa mapinduzi hayo yaliyofeli. Katika mkanda huo wa video ambao ulichukuliwa mjini Istanbul, askari wachinjaji walisikika wakisema kama ninavyonukuu: "Tumewaua wanne na huyu ni watano". Hawa ni mbwa. Hawa ni makafiri", mwisho wa kunukuu.
Kwa upande wake gazeti la Suzjo la Uturuki liliripoti siku moja baadaye yaani siku ya Jumamosi ya tarehe 16 Julai kwamba, watu kadhaa waliokuwa na hasira waliwachinja askari mjini Istanbul na kwamba habari hizo hazikuripotiwa.
Ripoti hizo zimesababisha kuongezeka kwa hali ya wasiwasi kuhusu ukatili dhidi ya askari hao ambao hadi sasa wanaendelea kushikiliwa na serikali kusikojulikana.
Kwengineko Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ameamuru kufungwa shule binafsi zaidi ya 1000 sanjari na kujadidisha sharia ambayo kwa mujibu wake, baadhi ya washukiwa wa mapinduzi yaliyofeli watatiwa mbaroni bila kufunguliwa mashitaka. Hii ni amri ya kwanza kutolewa na rais huyo wa Uturuki tangu kulipotangazwa hali ya hatari ya miezi mitatu nchini humo.
Jumatano iliyopita Erdoğan alitangaza hali ya hatari na kutoa amri ya kuwatia mbaroni haraka sana washukiwa wote wa mapinduzi hayo yaliyofeli. Kwa akali watu 264 waliuawa katika mapinduzi hayo.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu amesema kuwa, serikali ya nchi yake imeazimia kumrejesha Fethullah Gülen na kwamba itaanza kuandaa taratibu zote za kisiasa na kisheria zitakazohakikisha Marekani inamkabidhi mtuhumiwa huyo kwa Uturuki. Çavuşoğlu amesisitiza kuwa, serikali yake haitorudi nyuma katika suala hilo la kutaka kumrejesha nchini Fethullah Gülen, kiongozi wa kidini na mpinzani wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan ambaye amekuwa akinyooshewa kidole cha tuhuma na rais huyo kwa kile kinachotajwa kuwa alihusika katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, hatma ya faili la kumrejesha Gülen itabainika baada ya siku 10 tokea sasa.