Zaidi ya mawaziri 40 wa Afrika wakutana nchini Russia
(last modified Sat, 09 Nov 2024 10:38:19 GMT )
Nov 09, 2024 10:38 UTC
  • Zaidi ya mawaziri 40 wa Afrika wakutana nchini Russia

Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano wa Russia na Afrika umeanza leo katika mji wa pwani wa Sochi, kusini mwa Russia; kuashiria muundo mpya wa kawaida wa mazungumzo kufuatia mikutano ya kilele kati ya pande mbili hizo.

Mkutano huo unaofanyika leo Novemba 9 na kesho Jumapili Novemba 10 kwa uenyeji wa Wakfu wa Roscongress, unawaleta pamoja zaidi ya mawaziri 40 kutoka bara Afrika.

Taarifa ya waandaaji wa mkutano huo iliyonukuliwa na shirika la habari la TASS imethibitisha kuwa, washiriki 1,500 wanashiriki mkutano huo, wakiwemo mawaziri wa mambo ya nje, uchumi, afya, maendeleo ya kidijitali, na elimu kutoka nchi kama vile Algeria, Angola, Nigeria, Ethiopia, Uganda, na wengine wengi.

Aidha wajumbe waandamizi kutoka Umoja wa Afrika na mashirika ya ushirikiano wa kikanda pia watahudhuria mkutano huo, pamoja na shakhsia kutoka sekta za biashara, fedha, wanafikra, na waandishi wa habari wa Russia na Afrika.

Rais Vladimir Putin wa Russia na viongozi wa Afrika mjini St Petersburg Oktoba 2024

Mada kuu zinazojadiliwa katika mkutano huo wa mjini Sochi ni pamoja na suala la ushirikiano wa kiuchumi, mikataba ya kibiashara na changamoto zinazozakabili nchi za Afrika hasa wanachama wa BRICS, kama vile mivutano ya kijiografia, mdororo wa uchumi wa dunia na mabadiliko ya tabianchi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita,  viongozi wa Afrika waliohudhuria mkutano wa kilele wa mataifa ya BRICS nchini Russia walijikita katika kutoa mwito kwa taasisi za kimataifa kulitendea haki bara la Afrika.