Kushadidi hitilafu katika Umoja wa Ulaya
(last modified Tue, 12 Nov 2024 03:54:56 GMT )
Nov 12, 2024 03:54 UTC
  • Kushadidi hitilafu katika Umoja wa Ulaya

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekuwa zikikabiliwa na mizozo kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi, mizozo ambayo imezidi kuongezeka kutokana na kuendelea vita vya Russia na Ukraine, hivi kwamba sasa vita hivyo vimekuwa miongoni mwa migogoro mikuu zaidi katika umoja huo.

Katika muktadha huu, Olaf Scholz Kansela wa Ujerumani amekiri kuwepo mgawanyiko mkubwa katika Umoja wa Ulaya kuhusu suala la Ukraine na kuashiria tofauti kali zilizopo kati yake na Viktor Orban, Waziri Mkuu wa Hungary kuhusu suala zima la kuungwa mkono Kyiv katika vita na Russia.

Scholz amedokeza kuwa sio wanachama wote wa Umoja wa Ulaya wanaounga mkono msimamo maalum katika kushughulikia mzozo wa Ukraine, na kuongeza kuwa, maoni ya waziri mkuu wa Hungary kuhusu mzozo huo yanatofautiana sana na yale ya Ujerumani na nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Kuendelea vita nchini Ukraine sambamba na matukio ya kisiasa na kijeshi katika nyanja mbalimbali za kimataifa, kumefanya hali kuwa ngumu zaidi kwa viongozi wa Ulaya. Vita vya Ukanda wa Gaza na kuendelezwa kwake na utawala katili wa Israel na wajibu wa nchi nyingi za Ulaya wa kuunga mkono utawala huo, ushindi wa vyama vya mrengo wa kulia katika baadhi ya nchi za Ulaya na ushawishi mkubwa wa vyama hivyo katika mfumo wa maamuzi ya nchi za Ulaya, uchaguzi wa rais wa Marekani ambao sasa umemalizika kwa ushindi wa Donald Trump na vile vile kuongezeka suala la wahamiaji ni mambo ambayo yamewafanya viongozi wa Ulaya waendelee kutofautiana na hata mara nyingine kuwa na misimamo inayogongana kuhusu changamoto zinazowakabili, likiwemo suala la vita vya Ukraine.

Kuongezeka mivutano katika Umoja wa Ulaya EU.

Vita vya Russia na Ukraine vinapitia mwaka wake wa tatu huku Kyiv ikiwa haijapata mafanikio yoyote makubwa katika medani ya vita, licha ya kupewa misaada yote ya kijeshi na silaha na nchi za Magharibi. Shirika la Bloomberg limeandika katika ripoti kwamba, jeshi la Russia, likiwa na zana na silaha bora, linadhibiti moja ya tano ya ardhi ya Ukraine, huku jeshi la Ukraine likijitahidi kulinda vikosi na safu zake, na hii ni katika hali ambayo nchi za Ulaya zimetoa misaada mingi ya kifedha na silaha kwa Kyiv.

Suala la kuendelea misaada ya Ulaya kwa Ukraine sasa limekuwa mojawapo ya mambo makuu yanayojadiliwa katika Umoja wa Ulaya. Katika nchi nyingi za Ulaya, hali ya kiuchumi imekuwa ngumu kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya kijeshi pamoja na kukatwa gesi ya Russia. Kwa upande mwingine, baadhi ya nchi hizo pia zinaamini kuwa vita hivi vinaendelea kupoteza rasilimali za Ulaya bila kufikiwa natija yoyote hivyo zinataka mazungumzo yafanyike kwa lengo la kuvisimamisha kabisa.

Namna ya kujiunga Ukraine na NATO ni suala jingine linaloongeza mivutano ya viongozi wa Ulaya, jambo ambalo ni moja ya sababu kuu za kuanza vita vya nchi hiyo na Russia. Hata hivyo nchi nyingi za Magharibi bado ni watetezi wakuu wa Ukraine kupewa uanachama katika jumuiya hiyo ya kijeshi. Hii ni pamoja na ukweli kwamba Ukraine haina masharti yanayofaa kwa ajili ya kujiunga na kundi hilo la kijeshi.

Katika hali ambayo Hungary na Slovakia ni miongoni mwa wapinzani wakuu wa kuendelea misaada ya Ulaya kwa Ukraine, nchi nyingine za Ulaya, ikiwemo Ujerumani, zinasisitiza kuendelea kusaidiwa Ukraine kwa hali na mali. Waungaji mkono wa Ukraine wanaona kwamba kusitishwa misaada kwa nchi hiyo ni sawa na kudhoofishwa Ulaya na kukubali kushindwa katika vita hivyo. Lakini nchi kama Hungary zinaamini kuwa mkakati huu haukuwa sahihi tangu mwanzo na unapaswa kusimamishwa haraka iwezekanavyo.

Aidha msimamo tofauti wa Trump kuhusu vita hivi pia umeongeza wigo wa kutoelewana viongozi wa Ulaya kuhusu kuendelea misaada yao kwa Ukraine. Kuhusu suala hilo, Peter Siarto Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary amesisitiza kwamba,  Umoja wa Ulaya unapaswa kubadilisha mtazamo wake wa vita huko Ukraine. Amesema: 'Tunahitaji mkakati mpya kwa manufaa ya Ulaya ili kuzuia matatizo yanayotia wasiwasi.'

Ni wazi kwamba, kutokana na kuongezeka hitilafu katika Umoja wa Ulaya, jambo ambalo Kansela wa Ujerumani pia amelikiri waziwazi, umoja huo sasa unakabiliwa na tishio kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.