Miito ya kutimuliwa uwanachana Israel Umoja wa Mataifa yazidi kuongezeka
(last modified Wed, 13 Nov 2024 02:20:05 GMT )
Nov 13, 2024 02:20 UTC
  • Miito ya kutimuliwa uwanachana Israel Umoja wa Mataifa yazidi kuongezeka

Mataifa mbalimbali duniani yameendelea kutoa wito wa kufutiwa uanachama Israel katika Umoja wa Mataifa kutokana na jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina na Lebanon.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amesema kuwa, utawala ghasibu wa Israel unapaswa kufutiwa uwanachama katika Umoja wa Mataifa kutokana na jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina na chokochoko zake za kijeshi dhidi ya mataifa mengine ya dunia.

Akihutubia mkutano wa viongozi wa nchi za Kiislamu nchini Saudi Arabia, Waziri Mkuu wa Pakistan sambamba na kulaani jinai za Israel huko Gaza amesema, licha ya hukumu ya mahakama ya kimataifa dhidi ya jinai za kivita za utawala wa Kizayuni, utawala huu umeendelea kukiuka sheria na maadili ya kimataifa na umeua shahidi maelfu ya watu wasio na hatia na kuwafanya mamilioni ya watu kukosa makazi.

Miito ya kutaka kusimamishwa uwanachama Israel na hata kutengwa kimataifa imeongezeka mno katika miezi ya hivi karibuni. Hivi karibuni Amir Saeid Iravani, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alilihimiza Baraza Kuu la umoja huo lisimamishe uwanachama wa utawala ghasibu wa Israel kutokana na jinai unazoendelea kufanya dhidi ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina.