Idadi ya wafungwa Ufaransa yavunja rekodi huku wasiwasi wa msongamano ukiongezeka
Wasiwasi umeibuka katika magereza ya Ufaransa baada ya idadi ya wafungwa kuongezeka na kuibua wasiwasi wa kutokea msongamano katika magereza ya nchi hiyo.
Idadi ya wafungwa nchini Ufaransa iliongezeka zaidi mnamo Septemba 1, na watu 78,969 wamefungwa ikilinganishwa na wafungwa 78,397 mwezi wa kabla yake. Hiyo ni kulingana na Wizara ya Sheria ya Ufaransa.
Takwimu zilipungua kidogo mnamo Agosti baada ya kuongezeka kwa miezi kumi mfululizo iliyopita, na hivyo kupunguza kasi ya msimu katika shughuli za mahakama katika msimu wa joto.
Kufikia Septemba 1, wafungwa 3,609 walilazimishwa kulala kwenye godoro lililowekwa kwenye sakafu, ikilinganishwa na 2,361 mwaka uliopita.
Magereza ya Ufaransa yana nafasi 62,014 kwa jumla ambayo ina maana kuwa ni asilimia 127.3 juu ya uwezo wake.
Katika baadhi ya vituo, ambapo wafungwa wanasubiri kufikishwa mahakamani na wanaodhaniwa kuwa hawana hatia, au wamepewa hukumu fupi, idadi hii inaruka hadi asilimia 153.6.
Wakati mwingine huzidi asilimia 200 katika vituo 17 kote Ufaransa.
Ufaransa ina jumla ya magereza 188, vituo vya mahabusu na taasisi nyingine za adhabu.
Ufaransa ina moja ya rekodi mbaya zaidi barani Ulaya katika suala la msongamano wa wafungwa, kulingana na utafiti uliochapishwa mnamo Juni na Baraza la Ulaya.