Mahakama ya New York yamhukumu Trump katika kesi ya ufisadi
Mahakama ya New York jana ilitoa hukumu yake dhidi ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump katika kesi ya faili la ufisadi wa kingono.
Jaji Juan Merchan aliamua 'kumwachiliwa bila masharti' rais mteule wa Marekani, Donald Trump, siku chache kabla ya kuapishwa kwake Januari 20, katika kesi inayojulikana kama 'hush money', lakini Trump atakuwa rais wa kwanza kuchukua madaraka baada ya kuhukumiwa kwa kupatikana na hatia ya uhalifu.
Jaji wa kesi hiyo ameiambia mahakama kwamba ameamua kumwachiliwa bila masharti kuwa ndio "hukumu, bila kuingilia ofisi ya juu zaidi ya nchi."
Hata hivyo shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa katika hali ya kawaida, Trump angehukumiwa kifungo cha miaka minne jela.
Trump amepatikana na hatia ya makosa 34 ya kughushi nyaraka za biashara. Miongoni mwa tuhumu zilizokuwa zikimkabili Trump katika kesi hiyo ni jaribio la kuficha hati zinazohusiana na malipo ya fedha za kifumbamdomo, dola laki moja na elfu thelathini, ambazo wakili wake alimpatia mwigizaji wa filamu za ngono, Stormy Daniels kabla ya uchaguzi wa rais wa 2016. Pesa hizi zililipwa kwa Stormy Daniels ili kumzuia kufichua uhusiano wake haramu wa kingono na Donald Trump miaka michache iliyopita.