Rais wa Iraq asisitiza kuimarisha uhusiano na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133846-rais_wa_iraq_asisitiza_kuimarisha_uhusiano_na_iran
Rais wa Iraq amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2025-12-02T13:24:22+00:00 )
Dec 02, 2025 13:24 UTC
  • Mazungumzo ya Rais wa Iraq na balozi wa Iran mjini Baghdad
    Mazungumzo ya Rais wa Iraq na balozi wa Iran mjini Baghdad

Rais wa Iraq amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Abdul Latif Jamal Rashid wa Iraq amesema hayo katika mazungumzo yake na balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Baghdad.

Mohammad Kazem Al-Sadeq, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Baghdad amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Iraq Abdul Latif Jamal Rashid leo na wawili hao kubadilishana mawazo kuhusiana na uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo na kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais wa Iraq, mkutano huo ulifanyika katika Ikulu ya Baghdad. Mwanzoni mwa kikao hicho, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Shamal Jamal Rashid, kaka wa Rais wa Iraq, na kumuombea dua Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu na awape subira na uvumilivu familia yake.

Katika kikao hicho, Rais wa Iraq amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya Iraq na Iran na kuendelea mashauriano na uratibu baina ya nchi hizo mbili katika masuala mbalimbali yanayohusu masuala ya pamoja.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Baghdad sanjari na kumshukuru Rais wa Iraq amesisitiza azma ya nchi yake ya kutaka kuzidisha uhusiano wa pande mbili na kupanua upeo wa ushirikiano na Iraq katika nyuga mbalimbali kwa shabaha ya kuhudumia maslahi makubwa ya nchi hizo mbili jirani.