Ujerumani yajitutumua, yatoa onyo dhidi ya Marekani
(last modified Sat, 22 Feb 2025 11:55:04 GMT )
Feb 22, 2025 11:55 UTC
  • Ujerumani yajitutumua, yatoa onyo dhidi ya Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema Ulaya haipaswi kusita kuweka mashinikizo dhidi ya Marekani, iwapo Washington itashindwa kukumbatia 'demokrasia ya kiliberali'.

Annalena Baerbock ameyasema hayo kufuatia mazungumzo kati ya Marekani na Russia ambayo yamewatenga wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya na Ukraine.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni huko Potsdam jana Ijumaa, mwanasiasa huyo wa Chama cha Kijani alisema, "Tunaongeza mashinikizo kwa Wamarekani [ili wajue] wana mengi ya kupoteza ikiwa hawatasimama upande wa demokrasia huria za Ulaya."

"Hakuna anayeweza kuamua kuhusu vita na amani kwa Waukraine au sisi Wazungu (watu wa Ulaya), na huu ndio msimamo wa Wajerumani," amesisitiza Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Ujerumani.

Vita vya Ukraine

Weledi wa mambo wanasema, kurejea kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House ya Marekani kumevuruga kabisa matarajio ya viongozi wa Ulaya kuhusu vita vya Ukraine.

Trump ametumia mkanganyiko wa serikali za Ulaya kuhusu jinsi ya kukabiliana na vita vya Ukraine katika kuifedhehesha Ulaya, ambapo hata amezinyima fursa ya kushiriki katika mazungumzo na Russia.

Kadhalika Rais huyo wa Marekani hivi karibuni alishambulia vikali Rais Vladimir Zelensky wa Ukraine, na kumtaja kama "dikteta asiyechaguliwa."