Haki za binadamu; Chombo kinachohudumia maslahi ya kitaifa ya Marekani
Moja ya nyadhifa muhimu za kutumia haki za binadamu kama wenzo katika sera ya mambo ya nje ya Marekani ni kuhalalisha sera za nchi hiyo katika sehemu mbalimbali za dunia.
Kutetea haki za binadamu katika maneno na matamshi tu na kuzikiuka kivitendo kumezigeuza haki za binadamu kuwa chombo kinachohudumia na kudhamini maslahi ya kitaifa ya Marekani. Marekani daima imekuwa ikijitangaza kama mtetezi wa haki za binadamu katika sera yake ya kigeni. Wakati huo huo, hatua za nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya dunia, ikiwa ni pamoja na uvamizi wake huko Afghanistan na Iraq na kuweka vikwazo vya muda mrefu dhidi ya nchi zinazopinga sera za kibeberu za Washington, vimesababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na katika baadhi ya matukio, zimepelekea kutekelezwa jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Uchunguzi wa vitendo vya Marekani, katika sera za ndani na za kigeni, unaonyesha kwamba Washington inazitazama haki za binadamu kama chombo na wenzo wa kufikia maslahi yake. Hapa linajitokeza swali kwamba, haki za binadamu zina nafasi gani katika mfumo wa sera za kigeni za Marekani?

Ili kujibu swali hili, lazima tuseme kwamba, Marekani ni mojawapo ya nchi chache ambazo zina sera ya kigeni ya kiaidiolojia. Tofauti ni kwamba, mara nyingi, kama vile katika kulinda haki za binadamu, kukuza demokrasia na kulinda amani, sera ya kigeni ya kiitikadi (ideological foreign policy) hutumiwa kama chombo cha kulinda maslahi ya kitaifa ya Marekani. Kwa mfano, Marekani ilihalalisha mashambulizi yake makubwa ya kijeshi dhidi ya Afghanistan na kuikalia kwa muda mrefu nchi hiyo kwa kisingizio cha kukuza demokrasia. Hata hivyo, zaidi ya miongo miwili baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo na baadaye kuondoka kwa madhila au tuseme "kukimbia" Afghanistan mwaka 2021, vinaonyesha kuwa matamshi na maneno kama vile kustawisha demokrasia, ni mambo yanayotumiwa kurembesha sera za nje ya nchi hiyo.
Katika miongo kadhaa iliyopita, haki za binadamu pia zimekuwa chombo cha mashinikizo dhidi ya nchi shindani au zinazopinga sera na siasa za kibabe na kikoloni za Marekani. Wakati wa Vita Baridi, "haki za binadamu" zilitumiwa na Marekani na washirika wake kama chombo na silaha ya kupenya na kuvuka pazia la chuma la Muungano wa Soviet na kumuweka mpinzani wao huyo mkubwa katika hali ya kujilinda badala ya kushambulia. Marekani na washirika wake wa Kimagharibi wameendelea kutumia haki za bindamu kama wenzo na silaha dhidi ya wapinzani au washindani wao katika vipindi vya baada ya Vita Baridi.

Naam, katika maneno na matamshi yao, maafisa wa serikali ya Marekani wanajionyesha kama watetezi wa maadili na haki za binadamu, lakini kivitendo, hawatosheki kukanyaga na kuzichinja haki hizo za binadamu, bali pia wanaanzisha uhusiano wa karibu na nchi zinazokiuka haki za binadamu, na hata kuwakingiai kifua makatili na watu waovu kama Netanyahu waliotajwa na mahakama za kimataifa kuwa ni watenda jinai za kivita na dhidi ya binadamu, na wanasakwa kwa makosa ya kufanya mauaji ya kimbari.