Iran yasisitiza kuhusu kulindwa misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa
Katika mkutano wa ngazi ya juu wa Kundi la Marafiki wa Kulinda Mkataba wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Moscow, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisheria na kimataifa, Kazem Gharibabadi, amesisitiza umuhimu wa kufufua mfumo wa kimataifa wa pande nyingi (multilateralism) na kulinda misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Akizungumza mbele ya wawakilishi kutoka nchi 20, Gharibabadi alikosoa ongezeko la “utaratibu wa upande mmoja (unilateralism) kupita kiasi,” hasa kutoka mataifa yenye nguvu, na kuongeza kuwa hali hiyo inahujumu sheria za kimataifa na kudhoofisha mifumo ya uongozi wa dunia.
Ameonya kuwa kuna hatari ya walimwengu kutokuwa na imani tena na Umoja wa Mataifa kutokana na utekelezaji wa mapendeleo wa kanuni za kimataifa na matumizi ya taasisi za UN kama vyombo vya shinikizo la kisiasa.
Akitoa mfano wa vita vya Israel dhidi ya Gaza, Gharibabadi amelaani kushindwa kwa Baraza la Usalama la UN kuzuia kile alichokitaja kuwa vita vya mauaji ya kimbari vinavyoungwa mkono na Marekani. Amesema hatua hiyo inatokana na vizuizi vya makusudi vinavyowekwa na mataifa yanayokaidi Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Akitetea msimamo wa Iran wa kuunga mkono mfumo wa pande nyingi, alitoa wito kwa Kundi la Marafiki kupitisha mikakati madhubuti, ikiwa ni pamoja na kukataa vikwazo vya upande mmoja, kutetea mamlaka ya kitaifa, kukuza suluhu za kidiplomasia, na kushinikiza mageuzi ndani ya UN, hususan Baraza la Usalama.
Mkutano huo pia ulijadili masuala mapana ya kisiasa, yakiwemo mabaki ya ukoloni na mizozo ya Palestina na Ukraine. Washiriki wamesisitiza haja ya mfumo wa kimataifa unaoongozwa na sheria, heshima ya pande zote, na ushirikiano—hasa kwa mataifa ya Kusini mwa Dunia yanayotafuta kurekebisha mfumo wa dunia usio na usawa unaoongozwa na mataifa ya kihegemonia.
Kundi la Marafiki wa Kulinda Mkataba wa Umoja wa Mataifa limeibuka kama jukwaa la upinzani wa pamoja dhidi ya vikwazo visivyo halali, uingiliaji wa ajinabi, na shinikizo la kijiografia, likitetea badala yake ujumuishaji, heshima ya pande zote, na ushirikiano wa kimataifa unaozingatia sheria.