UN yapinga kuondolewa Taliban kwenye orodha iliyopigwa marufuku ya Russia
(last modified Sat, 19 Apr 2025 02:21:52 GMT )
Apr 19, 2025 02:21 UTC
  • UN yapinga kuondolewa Taliban kwenye orodha iliyopigwa marufuku ya Russia

Kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Russia wa kuliondoa kundi la Taliban kwenye orodha ya mashirika yaliyopigwa marufuku, Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba hatua hiyo haibadilishi hadhi ya Taliban katika taasisi hiyo na kwamba vikwazo vya kimataifa dhidi ya kundi hilo vitaendelea kuwepo.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa Russia wa kuliondoa kundi la Taliban kwenye orodha ya mashirika yaliyopigwa marufuku hautakuwa na taathira katika hadhi ya kundi hilo kimataifa.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema: "Huu ni uamuzi huru wa Shirikisho la Russia. Hadhi ya Taliban katika Umoja wa Mataifa, kama ilivyoamuliwa na nchi wanachama, bado haijabadilika."

Hapo awali, Mahakama Kuu ya Russia ilikuwa imekubali ombi la Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa nchi hiyo kuliondoa kundi la Taliban kwenye orodha ya mashirika yaliyopigwa marufuku. Kwa mujibu wa uamuzi huo, marufuku ya shughuli za Taliban nchini Russia imeondolewa mara moja.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesisitiza kuwa uamuzi huo haubadilishi wajibu wa Moscow kwa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Taliban imekaribisha hatua ya Russia. Zabihullah Mujahid, msemaji wa serikali ya Taliban amepongeza mwelekeo wa Rais Vladimir Putin wa Russia na kusema Taliban inatumai kupanuliwa uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya pande hizo mbili.