Mabadiliko ndani ya Ikulu ya White House, ni zaidi ya marekebisho madogo
Kufutwa kazi kwa Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani, Michael Waltz na naibu wake, Alex Wong, na kuteuliwa Marco Rubio, kama Kaimu Mshauri wa Usalama wa Taifa, kumekuwa na mwangwi mkubwa.
Trump ameandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba: "Ninafuraha kutangaza kwamba nitamteua Mike Waltz kama mwakilishi ajaye wa Marekani katika Umoja wa Mataifa. Tangu wakati alipohudumu kwenye uwanja wa vita akiwa amevalia sare, hadi wakati alipokuwa katika Congress, na kisha kama Mshauri wangu wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz daima alifanya jitihada za kuweka mbele maslahi ya nchi yetu. Nina hakika kwamba, atafanya vivyo hivyo katika majukumu yake mapya.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio atahudumu kama Kaimu Mshauri wa Usalama wa Taifa, huku akiendelea na majukumu yake ya kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje."
Hata hivyo, wanataalamu wa masuala ya Marekani wanatathmini na kuchambua mabadiliko haya kuwa ni zaidi ya marekebisho madogo tu katika Ikulu ya White House. Kufutwa kazi Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Mike Waltz, na uteuzi wa muda wa Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, kushika nafasi hiyo ni jambo ambalo limepokewa kwa jicho la shaka, wasiwasi na uchambuzi, huko Washington na katika miji mikuu ya washirika wa Marekani. Kidhahiri inaonekana kuwa, kufichuliwa bila kukusudia kwa maelezo ya siri katika kikundi cha ujumbe uliosimbwa kunatajwa kuwa sababu kuu ya kutimuliwa Waltz. Lakini wafuatiliaji wa muundo wa mamlaka ndani ya Ikulu ya Rais wa Marekani wanajua kwamba, tukio hilo ni zaidi ya makosa ya kiufundi.
Taarifa zilizovuja kutokana na makosa ya Michael Waltz zinahusiana na mipango ya operesheni za kijeshi za Marekani nchini Yemen. Ijapokuwa tukio hili si jipya katika mazingira rasmi ya usalama ya Marekani, lakini hatua ya haraka ya Trump inaashiria unyeti wa suala hilo kwa mtazamo wa kisiasa, na sio wa usalama tu. Kutolewa ripoti kuhusu hatua ya Mshauri wa Usalama wa Taifa kutumia barua pepe ya kibinafsi kwa ajili ya mawasiliano nyeti kumechochea tu moto wa mgogoro uliokuwa ukitokota. Afisa wa zamani wa usalama wa taifa anasema: "Waltz alitaka kuchukuliwa msimamo mkali zaidi kuhusu Iran, lakini Trump anataka kubakisha anga ya mazungumzo. Hitilafu hizi zimeshindwa kutatuliwa."
Katika muktadha huo, Richard Haas, rais wa zamani wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni, ametahadharisha kuhusu mabadiliko ya ndani ya Ikulu ya White House akisema: "Iwapo Rubio atataka kutekeleza majukumu mawili kwa wakati mmoja, anaweza kuingia katika mtego wa siasa za kijazba. Marekani haiwezi kumudu kuingia katika vita vingine Mashariki ya Kati."
Kuteuliwa haraka Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje na mwaminifu wa kisiasa wa Trump, Kama kaimu Mshauri wa Usalama wa Taifa ni hatua inayokumbusha enzi za Nixon na Henry Kissinger. Hata hivyo kuna tofauti muhimu kati ya hali hizi mbili: Kissinger, kama mwanastatijia mbobezi na aliyekuwa na uhalali wa kitaasisi, alikuwa ameweka uwiano muhimu katika sera ya nje ya Marekani; wakati kuteuliwa Rubio, zaidi kunaonekana kama kutanguliza mbele uaminifu wa kisiasa kuliko ubobezi na utaalamu.
Katika muundo wa utawala wa Marekani, nafasi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa inafafanuliwa kwa kuratibu majukumu ambako kwa kawaida kunahitaji uhuru na kutokuwa chini ya Waziri wa Mambo ya Nje na Pentagon. Kuchanganya majukumu haya mawili (Waziri wa Mambo ya Nje na Mshauri wa Usalama wa Taifa) katika mtu mmoja kuna maana ya kufutwa mojawapo ya tabaka za uangalizi katika kupanga sera za usalama wa taifa.
Wachambuzi wengi wa Washington wanaiona hali hii kuwa ni sawa na kurejea kwenye zama za "diplomasia ya kibinafsi"; Hali ambayo inaweza kuondoa sera ya kigeni katika mkondo wa taasisi za kijadi na kuigeuza kuwa chombo na karata ya mazungumzo ya nyuma ya pazia au katika masuala ya uaminifu wa kisiasa.
John Bolton, mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani katika utawala wa kwanza wa Trump, amesema katika mahojiano kwamba: "Hili ni jaribio hatari. Wizara ya Mambo ya Nje na Baraza la Usalama wa Taifa zina majukumu tofauti. Kuunganishwa taasisi hizi mbili pamoja kunaweza kupelekea kuchukuliwa maamuzi ya kukurupuka ambayo hayajachambuliwa."
Alaa kulli hal inaonekana kuwa, mabadiliko yanayofanyika katika Ikulu ya White House ni kielelezo cha ushindani mkubwa baina ya watu wa karibu ya Trump, na mpambano kati ya wababe wa vita na watetezi wa suala ushirikishwaji mkubwa zaidi katika kukabiliana na migogoro mbalimbali katika nyanja za kisiasa, kiusalama na kiuchumi. Mabadiliko haya yatakuwa na taathira za viwango tofauti kwa harakati za kisiasa na kimataifa za Marekani.