RSF: Palestina ni eneo hatari zaidi kwa waandishi wa habari kutokana na ukatili wa Israel
(last modified Sun, 04 May 2025 02:44:21 GMT )
May 04, 2025 02:44 UTC
  • RSF: Palestina ni eneo hatari zaidi kwa waandishi wa habari kutokana na ukatili wa Israel

Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani imeadhimishwa Mei 3 huku waandishi wa habari wa Palestina wakiendelea kufanya kazi katika eneo hatari zaidi duniani, kutokana na kulengwa na utawala katili wa Israel katika mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza.

Shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF) limesema kuwa Palestina kwa sasa inatambuliwa kuwa eneo hatari zaidi duniani kwa wanahabari, kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza.

RSF imeripoti kuwa askari wa jeshi la Israel wamewaua karibu waandishi wa habari 200 katika miezi 18 ya kwanza ya vita hivyo, 42 kati yao wameuawa wakiwa kazini.

Ripoti hiyo imesema: “Wakiwa wamenaswa ndani ya ukanda huo, waandishi wa habari huko Gaza hawana hifadhi na wanakosa kila kitu, ikiwemo chakula na maji.”

Chombo hicho cha uangalizi wa vyombo vya habari kimekadiria kuwa utawala wa Israel unatetea na kuhalalisha uhalifu unaofanywa dhidi ya waandishi wa habari.

RSF imesema: “Katika Ukingo wa Magharibi, waandishi wa habari wananyanyaswa na kushambuliwa mara kwa mara na walowezi pamoja na askari wa Israel.”

Tangu Israel ianzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, Wapalestina zaidi ya 52,500 wameuawa na wengine wasiopungua 118,100 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliouawa na kujeruhiwa katika mauaji hayo ya kimbari ni wanawake na watoto wa Kipalestina.