Vita na Trump: Sasa Ulaya yatafuta washirika wa Asia na Pasifiki
(last modified Tue, 06 May 2025 02:43:42 GMT )
May 06, 2025 02:43 UTC
  • Vita na Trump: Sasa Ulaya yatafuta washirika wa Asia na Pasifiki

Hatua ya rais wa Marekani ya kuvuruga mfumo wa uhusiano wa kimataifa, imeulazimisha Umoja wa Ulaya kuamua kuimarisha uhusiano wake na nchi za Asia na Pasiriki kupitia jumuiya kama Trans-Pacific.

Gazeti la Financial Times limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa: Viongozi wakuu wa nchi za Ulaya na wanadiplomasia wanaona kuwa, kurejea madarakani Donald Trump huko Marekani ni kichocheo cha kufufua mpango uliokwama wa kuunda ushirikiano wa kimkakati kati ya Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kibiashara ya Pasifiki yaani Trans-Pacific.

Kwa mujibu wa Pars Today, baada ya Trump kuzipandishia ushuru bidhaa za nchi nyingine duniani, kila nchi imekuwa ikichukua hatua za kupambana na rais huyo wa Marekani na hivi sasa Umoja wa Ulaya umeamua kuimarisha uhusiano wake wa kibiasha na nchi za Asia na Pasifiki zikiwemo pia nchi za Canada, Japan na Mexico.

Katika mahojiano na Financial Times, Mkuu wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema kwamba pande zote mbili zinachunguza ni mambo gani yanahitaji kuboreshwa katika Shirika la Biashara Duniani ili kukabiliana na msukosuko uliojitokeza hivi sasa na jinsi gani zinapaswa kuwa na uhusiano wa karibu baina yao ili kufanikisha malengo yao.

Jumuiya ya Ushirikiano ya Trans-Pacific (TPP) ilianzishwa mwaka wa 2018 na inajumuisha nchi za Australia, Brunei, Canada, Chile, Japan, Malaysia, Mexico, New Zealand, Peru, Singapore, Uingereza na Vietnam. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Canada nayo imetangaza kuwa nchi hiyo imejitolea kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara na Ulaya na eneo la Indo-Pacific.