China yatangaza kuwa tayari kuzipatanisha India na Pakistan
(last modified Fri, 09 May 2025 02:21:17 GMT )
May 09, 2025 02:21 UTC
  • China yatangaza kuwa tayari kuzipatanisha India na Pakistan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameelezea wasiwasi wake kuhusu mvutano uliozuka kati ya India na Pakistan na kutangaza kuwa, Beijing iko tayari kuchukua jukumu amilifu la upatanishi ili kupunguza mzozo kati ya nchi hizo mbili jirani za kusini mwa Asia.

Kwa mujibu wa gazeti la Global Times, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, ametangaza msimamo wake juu ya matamshi ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Shahbaz Sharif kuhusu kuwalipizia kisasi wahanga wa mashabulizi ya India, akisema jana (Alkhamisi, Mei 8) kwamba, China ina wasiwasi na hali inayoendelea hivi sasa baina ya nchi hizo mbili.

Amesema: "India na Pakistan ni majirani na wataendelea milele kuwa majirani. Muhimu zaidi ni kwamba, nchi zote hizo mbili ni majirani pia wa China."

Akieleza kuwa China inapinga aina zote za ugaidi, Lin amezitaka nchi zote mbili kutanguliza mbele amani na utulivu, kuheshimu Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria nyingine za kimataifa, kudumisha utulivu na kuwa wavumilivu, sambamba na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kupelekea hali kuwa mbaya zaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya  China amebainisha pia kuwa Beijing iko tayari kushirikiana na jamii ya kimataifa kubeba jukumu amilifu la kupunguza mvutano uliopo kati ya India na Pakistan.

Kwa mujibu wa IRNA, serikali ya India ilitangaza katika taarifa yake ya Jumanne usiku kwamba jeshi lake lililenga kwa makombora maeneo tisa ya Kashmir inayodhibitiwa na Pakistan na kudai ni ngome za magaidi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Muhammad Asif amethibitisha kuwa ndege za kivita za nchi hiyo na vikosi vyake vya ulinzi wa anga vimefanikiwa kutungua ndege tano za kivita za India baada ya shambulio la makombora la India. Waziri wa Ulinzi wa Pakistan amesema pia kuwa, madai ya New Delhi ya kwamba imelenga vituo vya magaidi hayana msingi wowote na ni upotoshaji na amesisitiza kuwa lazima Pakistan italipiza kisasi.