Mipaka iliyoacha nyuma ubinadamu
Katika habari za karibuni kuhusu ukiukwaji wa haki za wahamiaji na wakimbizi barani Ulaya, shirika la misaada la SOS Humanity, limetoa ripoti iliyopewa jina la "‘Borders of (In)Humanity’," ambayo imechapisha mahojiano na wakimbizi 64 waliookolewa baharini, na kufichua ukubwa wa janga la safari za vifo za wakimbizi kutoka Afrika kwenda Ulaya.
Leo huko Ulaya, maneno kama vile "mtafuta hifadhi" na "mhamiaji" yamekuwa misemo inayorudiwa mara kwa mara. Lakini maneno haya sio tu lebo ambazo zinaweza kupuuzwa kwa urahisi. Nyuma ya maneno haya kuna hadithi za maumivu, kukata tamaa na mapambano ya kubakia hai.
Wakimbizi wanaokwenda Ulaya wakihepa vita na umaskini, hufanya hivyo wakitarajia mwanzo mpya; hata hivyo wanakabiliwa na ukweli mchungu zaidi ya shubiri ambao labda hawajawahi kukutana nao hata katika ndoto mbaya na za kutisha. Katika ulimwengu ambapo Umoja wa Ulaya unajiona kuwa kinara wa haki na maadili ya kibinadamu, sera za uhamiaji za bara hilo zimekuwa kitendawili tata kilichojaa migongamo.
Ripoti ya hivi majuzi ya SOS Humanity, iliyopewa jina la "Mipaka (isiyo na) Ubinadamu," (Borders of (In)Humanity) imefichua ukweli mchungu. Kwa kutoa mamlaka ya udhibiti wa mipaka kwa nchi kama Libya na Tunisia, Ulaya sio tu imesahau wajibu wake wa kuwalinda wakimbizi, lakini pia imechochea, kwa njia isiyo ya moja kwa moja, ukiukwaji wa haki za binadamu. Bahari ya Mediterania, ambayo hapo awali ilikuwa nembo ya ustaarabu na daraja la kuunganisha tamaduni mbalimbali, leo imekuwa njia mbaya zaidi ya uhamiaji duniani. Takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) zinaonyesha kuwa, mwaka 2024 pekee, zaidi ya wahamiaji 2,333 walitoweka au kufariki dunia katika maji hayo. Lakini kinachofanya janga hili kuwa chungu zaidi ni nafasi na mchango usio wa moja kwa moja la Ulaya.

Ripoti ya SOS Humanity inaonyesha kuwepo ushirikiano wa walinzi wa pwani wa Libya na Tunisia na wasafirishaji haramu wa binadamu; Taasisi ambazo Umoja wa Ulaya umezikabidhi jukumu la kufuatilia wahamiaji kwa kufunga nazo mikataba ya mpaka. Watu waliotoa ushuhuda wametoa maelezo ya "mitandao ya uhalifu wa kupangwa" ambayo inaweka kizuizini, kutesa na hata kuwauza wahamiaji kama watumwa. Ripoti ya SOS Humanity inaelezea hali ya kutisha ambayo wakimbizi wanapitia wakiwa huko Libya na Tunisia. Kuanzia mateso ya kimwili na kisaikolojia hadi unyanyasaji wa kingono na njaa kali, mazingira ambayo ndani yake, wanadamu wamesahau thamani ya maisha na kupambana tu kwa ajili ya kubakia hai.
Hali katika vituo vya kuzuia wakimbizi na wahajiri vya Libya ni ya kutisha sana kiasi kwamba mashirika ya kutetea haki za binadamu yanalinganisha vituo hivyo na "kambi za kifo": njaa, mateso, mauaji ya watu wengi, na unyanyasaji wa kingono ni maisha ya kila siku ya wahamiaji katika kambi hizo.
Kinachozidisha mgogoro huo ni ushirikiano wa Umoja wa Ulaya (EU) na nchi zilizokumbwa na mzozo ambazo zenyewe zimekuwa sehemu ya tatizo hilo. Walinzi wa Pwani ya Tunisia na Libya, wanaofadhiliwa na kupewa vifaa na Umoja wa Ulaya, sio tu kwamba wameshindwa kuzuia wahamiaji kuvuka na kuelekea Ulaya, lakini katika baadhi ya matukio wameshirikiana na wasafirishaji na wafanya magendo ya binadamu. Huu ni ukweli mchungu unaoonyesha kwamba, sera za Ulaya sio tu zimeathiri vibaya haki za binadamu za wakimbizi, lakini pia zimewezesha kwa njia isiyo ya moja kwa moja biashara haramu ya binadamu.
Hali mbaya zaidi inashuhudiwa kwa watoto wahamiaji. Kundi la Lost in Europe limeripoti kuwa, zaidi ya watoto 51,000 wahamiaji wasio na walezi wametoweka barani Ulaya katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Takwimu hizi za kutisha zina maana kwamba, takriban watoto 47 hutoweka kila siku, na aghlabu huangukia mikononi mwa wafanya magendo ya binadamu na mitandao ya uhalifu. Watoto hawa, walio katika mazingira magumu sana, sio tu kwamba wananyanyaswa kimwili na kisaikolojia, lakini pia katika ulimwengu wa sasa, wanaweza kuwa bidhaa ya kibiashara katika soko la biashara haramu ya viungo vya binadamu.
Hivi sasa, wakati Ulaya inajiona kama chimbuko na chanzo cha haki za binadamu na demokrasia, inakabiliwa na swali kubwa, lini kauli mbiu hizo za kutetea demokrasia na haki za binadamu zitatekelezwa kivitendo kwenye mipaka ya Ulaya? Katika hali ya sasa ambapo Bahari ya Mediterania imekuwa kaburi la umati la wahamiaji, na katika kambi kama Moria nchini Ugiriki, maelfu ya watu wanaishi katika mazingira kama ya wanyama, ni vipi Umoja wa Ulaya unaweza kuendelea kutekeleza majukumu yake kama mtetezi wa haki za binadamu?
Kukua kwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya, kama vile Alternative for Germany (AfD) au Chama cha Uhuru cha Austria, kumemezielekkeza serikali kwenye siasa kali zaidi. Nchini Ujerumani, mijadala kama vile kufukuzwa kwa umati wakimbizi au kupunguzwa misaada yao ya kijamii imeongezeka sana kutokana na kuungwa mkono na mirengo hiyo. Sasa suluhisho ni lipi?

Maadamu serikali za nchi za Ulaya zinayapa makundi ya nje mamlaka ya kuingiza na kufukuza wahamiaji nje ya mipaka ya Ulaya, Bahari ya Mediterania itaendelea kuwa kaburi la maelfu ya wanawake, wanaume na watoto ambao dhhambi yao pekee ni kutafuta maisha bora ya baadaye.