Ansarullah: Tutavigeuza Jahannam viwanja vya ndege vya Israel
(last modified Fri, 09 May 2025 03:04:33 GMT )
May 09, 2025 03:04 UTC
  • Ansarullah: Tutavigeuza Jahannam viwanja vya ndege vya Israel

Vyombo vya habari vilivyoko karibuni na Ansarullah ya Yemen vimesambaza mkanda wa video unaotishia kulengwa viwanja vya ndege vya utawala ghasibu wa Kizayuni na kuvigeuza Jahannam na harakati hiyo.

Jeshi la Yemen limetangaza kuwa litaendelea kutoa vipigo kwa utawala wa Kizayuni hadi pale Israel itakapokomesha jinai zake huko Ghaza na kuacha kuuzingira ukanda huo. 

Wakati Israel ilipofikia makubaliano ya kusitisha vita na HAMAS, jeshi la Yemen nalo lilisitisha mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni.

Hivi sasa lakini wanamapambano wa Yemen wamerejea kuyapiga maeneo muhimu ya Israel zikiwemo bandari na viwanja vya ndege sambamba na kuvipiga marufuku vyombo vya baharini vinavyokwenda Israel visitumie Bahari Nyekundu baada ya utawala ghasibu wa Kizayuni kuanza tena kufanya jinai huko Ghaza.

Kabla ya hapo pia, Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen alitangaza kuwa nchi hiyo imefanya operesheni nyingine mbili za kijeshi kwa kutumia ndege zisizo na rubani kupiga maeneo mengine muhimu ya utawala wa Israel.

Msimamo thabiti wa Sana'a wa kuiunga mkono Ghaza umewahamakisha sana maafisa wa Israel. Waziri wa Vita wa Israel, Yisrael Katz amesema iwapo Wayemen wataendelea kuupiga utawala wa Kizayuni watapata pigo kubwa na kwamba eti jeshi la Israel limejipanga kwa kila hali.

Lakini Marekani ambayo ilianzisha vita kujaribu kuzuia mashambulizi ya Yemen imelazimika kuomba kusitisha vita na Ansharullah kutokana na hasara kubwa iliyopata Washington na kushindwa kuzuia mashambulizi dhidi ya Israel na wala kufungua njia ya baharini ya kupitisha bidhaa ziendazo kwa Wazayuni.