Je, Dan Jarvis anasema nini? Ni nani na amefanya nini?
Madai yaliyotolewa katika bunge la Uingereza siku ya Jumanne, Mei 6 na Dan Jarvis, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, kwa mara nyingine tena yameibua kile kinachodaiwa kuwa tishio la usalama kutoka Iran.
Kadhia hiyo inahusiana na kukamatwa kwa raia kadhaa wa Iran katika operesheni za hivi karibuni za kukabiliana na ugaidi nchini Uingereza, ikidaiwa kwamba Tehran imekuwa nyuma ya "njama kadhaa hatari" katika nchi hiyo katika miaka ya hivi karibuni. Dan Jarvis amedai kuwa raia watano wa Iran wametiwa mbaroni kwa tuhuma za "kutayarisha operesheni za kigaidi" na wengine watatu kwa tuhuma za kufanya kazi chini ya "Sheria ya Usalama wa Taifa." Bila kutoa maelezo zaidi au nyaraka zozote kuhusu kesi hizo, Jarvis amesema uchunguzi unaendelea na kukataa kutoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo kwa madai ya sababu za kiusalama. Pia amesema wafungwa watatu wa hivi karibuni ndio watu wa kwanza kulengwa na polisi chini ya sheria mpya ya usalama wa taifa, chini ya kipengele cha "vitishio vya serikali."
Afisa huyo wa Uingereza amedai kuwa Iran imekuwa ikijaribu kutekeleza vitendo vya mabavu katika ardhi ya Ulaya kupitia mitandao ya niaba, ukiwemo mtandao unaoitwa "Foxtrot" ambao Uingereza inadai kuwa una uhusiano na Iran, na ambao tayari umewekewa vikwazo. Sehemu ya matamshi yake ilihusu mpango mpya wa serikali ya Uingereza wa kusajili shughuli zote zinazohusiana na vyombo vya serikali za kigeni, na kusisitiza: "Yeyote anayefanya kazi na serikali ya Iran nchini Uingereza na asijiandikishe atakuwa amefanya uhalifu mkubwa."
Madai hayo yametolewa na afisa huyo wa Uingereza katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikikanusha tuhuma za aina hiyo. Alireza Yousefi, Naibu Waziri na Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Ulaya Magharibi katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni amekanusha tuhuma hizo na kusema: "Tabia inayokera ya baadhi ya wanasiasa na maafisa wa Uingereza ya kurudiarudia madai yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila shaka inaharibu uhusiano wa nchi mbili na kuchochea dhana mbaya ya kihistoria ya Wairani dhidi ya serikali ya Uingereza."
Tuhuma hizo za maafisa wa Uingereza dhidi ya Iran si suala geni na zimekuwa zikikaririwa kwa miaka mingi, hasa nyakati ambazo uhusiano wa nchi hizi umekuwa ukishuhudia mivutano. London mara kwa mara imeelezea wasiwasi wake kuhusu kile inachokiita "shughuli mbaya" za Iran kieneo na kimataifa. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha mara kwa mara tuhuma hizo na kuzitaja kuwa zisizo na msingi. Viongozi wa Iran mara nyingi wanayachukulia madai hayo kuwa sehemu ya propaganda na kampeni za mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Tehran, yanayofuatiliwa na nchi za Magharibi kwa malengo maalumu. Iran pia imewataka maafisa wa Uingereza kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo, jambo ambalo halijafanyika hadi sasa.

Suala muhimu linalohitaji kuchunguzwa ni historia ya afisa wa Uingereza anayetoa shutuma hizo zisizo na msingi dhidi ya Iran, Dan Jarvis, ambaye amechukua mkondo usio wa kawaida katika siasa za Uingereza akiwa mwakilishi wa Chama cha Labour na Waziri Kivuli wa Sheria. Kabla ya kuingia bungeni, alikuwa afisa wa jeshi, akihudumu katika operesheni hatari nchini Afghanistan na Iraq. Jarvis alikuwa na umri wa miaka 34 alipohudumu jeshini huko Kosovo, Ireland ya Kaskazini na Sierra Leone, na kufanya safari nyingi za kikazi nchini Afghanistan na Iraq. Aliongoza kikosi cha askari wa miamvuli cha Uingereza katika jimbo la Helmand, Afghanistan, mwaka 2007. Kitengo chake, kilichoundwa na askari wa miamvuli, kilikuwa sehemu ya Kundi la Kusaidia Vikosi Maalum, tawi jipya zaidi la vikosi maalumu vya Uingereza. Aliajiri pamoja na kuwafundisha wale waliojitolea kuhudumu katika vikosi vya nchi kavu huko Afghanistan; kitengo kilichopewa jukumu la kukabiliana na Taliban. Ripoti nyingi zimechapishwa hadi sasa kuhusu vitendo vya uhalifu vilivyofanywa na askari wa nchi za Magharibi, hasa wa Marekani na Uingereza, huko Afghanistan wakati wa uvamizi wa nchi hiyo kutoka 2001 hadi 2021.
Gazeti la Sunday Times liliripoti mwezi Mei 2024 kwamba vikosi maalum vya Uingereza vilishutumiwa kwa kufanya mashindano ya mauaji na kuweka silaha kwenye miili ya wahanga wa Afghanistan. Nyaraka zilizovuja zilionyesha kuwa mmoja wa maafisa wakuu wa kikosi maalum katika jeshi la Uingereza aliripoti kwa polisi kwamba wanajeshi waliokuwa chini yake walifanya uhalifu wa kivita kwa kuwaua bila makosa, wafungwa nchini Afghanistan. Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Times, afisa huyo aliwaambia wachunguzi wa Polisi wa Jeshi la Kifalme kwamba "saratani" ilikikumba Kikosi Maalum cha Uingereza, na kusababisha mauaji ya wafungwa kadhaa wa Afghanistan ambao hawakuwa na silaha. Kulingana na ripoti hiyo, afisa huyo alikuwa na wasiwasi kwamba kama askari wa kikosi maalum cha Uingereza wangegundua kwamba alikuwa amefichua suala hilo, wangelipiza kisasi kwa kuchukua hatua kali dhidi ya familia yake.
Kwa hakika kadhia ya kuuliwa raia wa Afghanistan na vikosi maalum vya Uingereza ni moja ya kesi muhimu zaidi za uhalifu wa kivita nchini Afghanistan, na bila shaka Dan Jarvis, ambaye sasa anaituhumu Iran, alikuwa mmoja wao. Ni wazi kuwa katika taarifa zake, haashirii hata kidogo vitendo vya uhalifu ambavyo yeye na ndugu zake walihusika navyo katika nchi hiyo. Miongoni mwavyo ni mauaji yaliyofanywa na vikosi maalum vya Uingereza vinavyotuhumiwa kuua takriban watu 80 katika jimbo la Helmand, ambao inadaiwa waliuawa kinyama, ama wakiwa usingizini au baada ya kukamatwa, kati ya 2010 na 2013. Gazeti la The Guardian hivi karibuni liliripoti kuwa uchunguzi wa kesi hii umeahirishwa na Wizara ya Ulinzi ya Uingereza hadi mwishoni mwa mwaka huu. Katika kesi hiyo hiyo, gazeti la Politico liliripoti kwamba Johnny Mercer, Waziri wa Uingereza wa Masuala ya Maveterani, ambaye alishikilia wadhifa huo hadi Julai 5, 2024, anaweza kuhukumiwa kifungo cha jela katika kesi ya uhalifu wa kivita. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, anakabiliwa na uwezekano wa kuadhibiwa na mahakama kwa kukataa kutaja watoa habari wa kijeshi waliomfahamisha kuhusu mauaji ya wanaume na watoto wa Afghanistan, yaliyofanywa na vikosi maalum vya jeshi la Uingereza.