Raia 5 wauawa katika mashambulizi ya India huko Kashmir
(last modified Fri, 09 May 2025 11:05:10 GMT )
May 09, 2025 11:05 UTC
  • Raia 5 wauawa katika mashambulizi ya India huko Kashmir

Mashambulizi ya India katika eneo la Kashmiri linalotawaliwa na Pakistan yamewaua raia watano. Mauaji hayo yanaripotiwa kufuatia siku kadhaa za makabiliano makali kati ya India na Pakistan katika eneo la Kashmir.

Vifo hivyo vimeripotiwa katika maeneo karibu na mpaka wenye shughuli nyingi za kijeshi unaofahamika kama Msitari wa Udhibiti unaolitenganisha eneo la Kashmir kati ya India na Pakistan.

Mjini Muzaffarabad, makao makuu ya Kashmir inayotawaliwa na Pakistan, afisa wa cheo cha juu ambaye hakutaka kutajwa majina amethibitisha kutokea vifo hivyo huko Kotli na kuongeza kwamba, mtu wa tano ameuawa katika wilaya ya Bagh.

Hayo yanajiri siku moja tu baada ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif kusema kwamba, nchi hiyo "italipiza kisasi cha damu za mashahidi wetu wasio na hatia" baada ya watu wasiopungua 31 kuripotiwa kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio ya India kwenye mkoa wa Punjab na Kashmir inayodhibitiwa na Pakistan.

Mvutano huo umekuwa ukiongezeka tangu Aprili 22 mwaka huu, kufuatia shambulio la kigaidi huko Pahalgam katika eneo la Jammu na Kashmir na kuuawa watu 26, huku Pakistan ikisema kuwa ipo tayari kwa uchunguzi wa kimataifa kuhusu hujuma hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu operesheni za kijeshi zinazofanywa na jeshi la India kwenye mstari wa usimamizi na mpaka wake wa kimataifa na Pakistan.

Viongozi na wanasiasa mbalimbali duniani wameendelea kuzitokea mwito India na Pakistan zijizuie na kutoshadidisha mgogoro huo amba oni tisho kwa usalama wa bara Hindi na Asia kwa ujumla.