Kamanda Mkuu wa IRGC: Iran itapiga popote patakapotumika kulenga maslahi yake
(last modified Fri, 09 May 2025 07:39:47 GMT )
May 09, 2025 07:39 UTC
  • Kamanda Mkuu wa IRGC: Iran itapiga popote patakapotumika kulenga maslahi yake

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami amesema Iran itapiga mahala popote ambapo adui atapatumia kuishambulia nchi hii.

Jenerali Salami alitoa onyo hilo jana Alkhamisi katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha chini ya ardhi cha ndege zisizo na rubani cha Jeshi la Wanamaji la IRGC wakati Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinatoa vitisho vya kuvishambulia vituo vya nishati ya nyuklia vya Iran.
 
"Kuna kanuni katika mwongozo wetu wa kiulinzi inayoeleza kwamba, mahali popote pale ambapo adui yetu atapatumia dhidi ya maslahi na malengo yetu, tutapalenga na kupapiga mahala hapo na mahala pengine popote yalipo maslahi ya adui yetu", amesisitiza Salami.
 
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kinagaubaga kwa kusema: "kwa hiyo, tunatangaza kuwa mahala popote katika ardhi yoyote patakapokuwa nukta ulipoanzia uvamizi patalengwa, kumaanisha kwamba mahala utapoanzia uvamizi patalengwa".
 
Wakati huohuo, Jenerali Salami amewahakikishia Wairani uwezo wa kijeshi wa nchi wa kukabiliana na tishio lolote lile na kusema: "wananchi wetu wapendwa inapasa wajue kwamba tumejizatiti kikamilifu dhidi ya maadui zetu".
 
Kituo cha chini ya ardhi cha ndege zisizo na rubani kilichozinduliwa siku ya Alkhamisi ndicho cha karibuni zaidi kuonyeshwa hadharani kati ya vituo kama hivyo vilivyoonyeshwa katika miezi ya hivi karibuni sambamba na chokochoko za kiusalama zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani, ambazo zimeitishia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa zitachukua hatua za kijeshi dhidi ya mpango wake wa nyuklia.
 
Akizungumzia kituo hicho, Jenerali Salami amesema: "kile ambacho wananchi wapendwa wa Iran wanashuhudia leo ni sehemu ndogo tu ya uwezo mkubwa wa Jeshi la Wanamaji la IRGC".../