Putin: Russia na China ni watetezi wa ukweli wa kihistoria
(last modified Thu, 08 May 2025 10:50:22 GMT )
May 08, 2025 10:50 UTC
  • Putin: Russia na China ni watetezi wa ukweli wa kihistoria

Moscow na Beijing zinaendelea kuwa watetezi thabiti wa ukweli wa kihistoria na zikikumbuka idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha katika nchi zao wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Rais Vladimir Putin wa Russia ameyasema hayo katika mazungumzo na Rais Xi Jinping wa China.

Xi ni miongoni mwa viongozi zaidi ya ishirini wa dunia wanaotarajiwa kuhudhuria mjini Moscow, matukio ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 ya ushindi wa Umoja wa Kisovyeti dhidi ya Ujerumani ya Kifashisti. Rais huyo wa China pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na maafisa wa Russia.

Katika mkutano uliofanyika Alhamisi, Putin alimshukuru “rafiki yake mpendwa” Xi kwa ziara yake na kwa kuungana naye katika kusherehekea “sikukuu takatifu kwa Russia.”

“Dhabihu ambazo mataifa yetu mawili yalitoa hazipaswi kusahaulika. Umoja wa Kisovyeti ulipoteza maisha ya watu milioni 27, waliotoa maisha yao kwa ajili ya Taifa na kwa ajili ya Ushindi. Na watu milioni 37 walipoteza maisha nchini China katika vita vyao vya kupigania uhuru na kujitegemea. Chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti, ushindi huu ulipatikana,” amesema.

Putin amesisitiza umuhimu wa ushindi dhidi ya ufashisti, akiongeza kuwa Russia na China “zinalinda ukweli wa kihistoria na kumbukumbu ya vita na zinapambana na dalili za sasa za neo-Nazism na uanajeshi.”

Kiongozi huyo wa Russia pia amemshukuru Xi kwa kumkaribisha kushiriki katika maadhimisho ya ushindi wa China dhidi ya Japan ya Kifalme katika Vita vya Pili vya Dunia.

Katika kauli zinazoendana, Xi amesisitiza kumbukumbu ya pamoja ya kihistoria na mshikamano wa kimkakati kati ya Beijing na Moscow.

Amebainisha kuwa: “Wachina na Warusi, kwa gharama ya kupoteza watu wengi, walipata ushindi mkubwa” na wakatoa “mchango wa kihistoria usiofutika kwa amani ya dunia na maendeleo ya binadamu."

Russia na China kwa muda mrefu zimekuwa na uhusiano wa karibu, huku nchi hizo mbili zikielezea mahusiano yao kama “ushirikiano usio na mipaka” ambapo “hakuna eneo lililopigwa marufuku.” Beijing pia imeendelea kukataa kuunga mkono vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow kuhusiana na mzozo wa Ukraine.