"Israel imehusika katika mapigano baina ya India na Pakistan"
(last modified Mon, 12 May 2025 05:48:00 GMT )
May 12, 2025 05:48 UTC

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimeripoti kuwa mabilioni ya dola za India katika ununuzi wa silaha kutoka Israel yamechangia pakubwa katika vita vya wiki iliyopita dhidi ya Pakistan.

Shirika la Habari la Tasnim limenukuu makala iliyoandikwa na gazeti la habari za kiuchumi la Calcalist la Israel ikisema kwamba mabilioni ya dola za India yaliyomiminwa kwenye viwanda vya silaha vya Israel kupitia manunuzi kama ya makombora na ndege zisizo na rubani zenye thamani ya dola bilioni kadhaa, katika miaka iliyopita, yamechangia pakubwa kwenye vita vya hivi karibuni kati ya India na Pakistan.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa: Mapigano kati ya majeshi ya India na Pakistan yalikuwa yamehamisha hisia za walimwengu kutoka kwenye jinai na mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina hasa Ghaza yanayoendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa huku makubaliano tete ya kusimamisha vita baina ya nchi hizo mbili yakiwa hayatoi dhamana yoyote ya kutozuka upya mapigano baina ya nchi hizo zinazomiliki silaha za nyuklia. Kwa muda fulani hisia za walimwengu zilitekwa na vita baina ya India na Pakistan.

Licha ya Marekani kutangaza kuwa imezipatanisha India na Pakistan na mapigano yamesimama, lakini jana nchi hizo mbili ziliendelea kushutumiana kuwa haziheshimu makubaliano hayo. Gazeti hilo la Kizayuni limesema kuwa, kuweko shehena kubwa ya silaha ambazo India imenunua kutoka kwa Israel, kunachangia hali tete iliyopo baina ya nchi hizo mbili jirani za kusini mwa Asia. 

Gazeti hilo la Israel limeandika: Moja ya silaha hizo ambazo India imenunua kutoka kwa utawala wa Kizayuni ni mfumo wa silaha za rununu wa "IAI Harop" ambao ni wa droni na ndege isiyo na rubani ya "kujiripua" yenyewe ambayo ina uwezo wa kupaa kilomita mia kadhaa na kubeba mabomu yenye uzito wa takriban kilo 10.