Kwa nini Marekani inafuatilia suala la kuongeza bajeti za kijeshi za wanachama wa NATO?
Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kufikia mkutano wa kilele wa NATO mwezi Juni mwaka huu, nchi zote wanachama wa muungano huo wa kijeshi zitakuwa zimekubaliana kutenga asilimia 5 ya pato lao la ndani kwa ajili ya ulinzi katika kipindi cha muongo mmoja ujao.
Marekani imezitaka nchi nyingi wanachama wa NATO kutia saini mikataba mipya na kujitolea kutumia fedha zaidi kabla ya mkutano wa Juni mjini The Hague. Takriban wakuu 45 wa nchi na serikali, akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani na viongozi wengi wa Ulaya, pamoja na mawaziri 90 wa mambo ya nje na ulinzi wapatao 90, watashiriki katika mkutano wa NATO mwezi ujao.
Kwa mujibu wa maafisa wa Uholanzi, mkutano huu ndio utakaokuwa mkutano mkubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini humo. Baada ya kumalizika kipindi cha Jens Stoltenberg (aliyekuwa Katibu Mkuu wa NATO), huu utakuwa mkutano wa kwanza wa NATO chini ya uongozi wa Mark Rutte, Waziri Mkuu wa zamani wa Uholanzi.
Ushahidi unaonyesha kuwa Trump ameweza kuzilazimisha nchi wanachama wa NATO kukubali kutenga asilimia 5 ya pato lao la ndani kwa ajili ya masuala ya kijeshi na ulinzi kupitia mashinikizo ya pande zote na kwa kuwatishia wanachama wa NATO kwamba Marekani ingechukua uamuzi wa kujiondoa katika muungano huo wa kijeshi, na pia kusimamisha uungaji mkono wake wa usalama kwa Ulaya kama haingekubali matakwa ya Washington. Trump anaamini kwamba kuongezwa bajeti hiyo kutapunguza pakubwa gharama ambazo Marekani huzitumia kwa ajili ya shughuli za NATO na uwepo wa majeshi ya Marekani barani Ulaya.
Ingawa NATO, ikiongozwa na Marekani, inaonekana kuwa na mshikamano wa kijeshi, lakini kisiasa kuna dalili zinazoonyesha kuwepo tofauti kubwa miongoni mwa wanachama wake. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, tofauti hizi zinasababishwa na utegemezi wa jadi wa Ulaya kwa Marekani katika kulilinda bara hilo na kukataa Trump kuendeleza suala hilo, na wakati huo huo kutoweza nchi za Ulaya kupitisha mkakati mmoja huru kuhusiana na Russia na vita vya Ukraine.
Wakati wa muhula wake wa kwanza madarakani kuanzia 2017 hadi 2021, Trump alilalamika mara kwa mara kwamba Marekani ilikuwa inagharamika zaidi ya wajibu wake katika NATO. Kabla ya kuchaguliwa kuwa rais kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa rais 2016, pia alikosoa upangaji wa bajeti ya muungano huo wa kijeshi. Wakati huo, Marekani ilikuwa ikilipa karibu asilimia 22 ya bajeti ya NATO, lakini Trump alitaka kupunguzwa mzigo huo hadi karibu asilimia 16. Licha ya kuwa na uchumi mkubwa, lakini Marekani ilijaribu kupunguza mzigo wake huo hadi kukaribia sehemu ya malipo ya Ujerumani, ambayo ilikuwa ikilipa asilimia 14.8 ya bajeti ya NATO.
Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikiwatuhumu washirika wake wa Ulaya kuwa wameshindwa kutenga asilimia 2 ya Pato la Taifa kwa matumizi ya ulinzi, lakini katika miezi ya hivi karibuni, na kutokana na kurejea Donald Trump katika Ikulu ya White House, sera za Washington zimeonyesha mabadiliko makubwa. Mwanzoni mwa muhula wake wa pili wa urais, Trump alitoa matakwa mengi mapya kwa wanachama wa NATO wa Ulaya akiwataka watenge asilimia 5 ya pato lao la taifa kwa ajili ya kugharamia shughuli za kijeshi za NATO. Takwa ambalo sasa anatumai kulitimiza katika mkutano wa kilele wa NATO huko The Hague mnamo mwezi ujao wa Juni.
Wataalamu wanaamini kuwa, tofauti zilizopo, pamoja na maslahi na vipaumbele tofauti vya Ulaya na Marekani, ni baadhi ya mambo ambayo yamefanya mustakabali wa ushirikiano katika mfumo wa NATO ukabiliwe na wasiwasi mkubwa. Tofauti hizi zinathibitisha wazi kwamba Ulaya ambayo inaitegemea pakubwa Marekani katika kudhamini usalama wake, inaingia katika hatua mpya ya mzozo wa kisiasa na kimkakati na Washington, hali ambayo inaweza kuibua changamoto kubwa kwa mshikamano wa ndani wa NATO katika siku zijazo.
Wakati huo huo, kutokana na kuongezeka pengo katika mahusiano ya pande mbili za Bahari ya Atlantiki, hasa baada ya Trump kuanzisha tena vita vya ushuru, na Ulaya kutuhumiwa kuwa inaitumia vibaya Marekani na kutokubaliana wazi na Washington kuhusu jinsi ya kukabiliana na Russia na kuhitimisha vita vya Ukraine, Ulaya sasa inatafuta zaidi njia za kujiimarishia ulinzi wake yenyewe kuliko wakati mwingine wowote. Kuhusiana na suala hilo, Tume ya Umoja wa Ulaya imekaribisha ongezeko la uwekezaji wa kijeshi hadi kufikia euro bilioni 800, na sambamba na hilo Ujerumani, ikiwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, imetangaza mipango ya kuwekeza euro trilioni moja kwa ajili ya kuboresha jeshi lake na kujenga upya miundombinu ya kiusalama.
Wakati huo huo, suala la kuongeza matumizi ya kijeshi katika nchi za Ulaya limepingwa vikali na wakosoaji hasa wa mrengo wa kushoto ambao wanahoji kuwa kuongezwa uwekezaji wa kijeshi kunaweza kudhuru ustawi wa watu wa nchi hizo. Hili lina ukweli wa aina fulani hasa ikitiliwa maanani hali ya nchi kama Uswidi ambapo "hali ya ustawi" inatawala. Kuhusiana na hili, baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa kutangulizwa masuala ya ulinzi na kijeshi kunaweza kupunguza matumizi na mipango ya kijamii na hivyo kuongeza ushawishi na nguvu za wanasiasa, harakati na vyama vya siasa kali barani humo.