Jeffrey Sachs: Marekani bado haikubali ukweli kuwa ubeberu wake umeisha dunaini
Mchumi mashuhuri wa Kimarekani, Profesa Jeffrey Sachs, amesema kuwa enzi ya Marekani kuwa dola kuu duniani imefikia kikomo, lakini Washington bado haijakubali ukweli huo.
Katika mahojiano na Shirika la Habari la TASS yaliyotolewa Jumamosi, Sachs alisema:“Tunaishi katika dunia ya ncha nyingi. Russia ni taifa lenye nguvu; Marekani ni taifa lenye nguvu; China ni taifa lenye nguvu; na India pia ni taifa lenye nguvu.”
Aliendelea kwa kuhoji:“Je, tunaweza kuishi kwa amani katika mazingira kama haya? Je, Marekani itakubali ukweli kwamba haiwezi tena kutoa maagizo kwa dunia?”
Sachs alisisitiza kuwa Marekani bado iko katika ‘hatua ya kutokubali’, na inadhani bado “ina satwa ya kibeberu.” Alionya kuwa hali hiyo ya kutokubali kuwa satwa yake imedidimia ni hatari kwa Marekani na kwa dunia nzima.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Profesa Sachs alizungumzia vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vilivyowekwa baada ya kuanza kwa vita vya Ukraine, akisema kuwa vikwazo hivyo, badala ya kuiangamiza Russia, vimeimarisha uchumi wake.
Alikiri kuwa vikwazo hivyo vimesababisha madhara fulani, lakini pia vimekuwa na matokeo chanya. Kwa mfano, mahusiano ya Russia na China pamoja na India yameimarika, na viwanda vya ndani ambavyo vilitegemea bidhaa za nje vimeanza kustawi kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani.
Marekani na washirika wake barani Ulaya wameweka vikwazo vikali dhidi ya Russia na maafisa wake tangu mwaka 2014. Vikwazo hivyo viliongezeka zaidi baada ya Russia kuanzisha kile inachokiita “operesheni maalum ya kijeshi” mashariki mwa Ukraine mnamo Februari 2022, ikiwa ni juhudi za kuzuia upanuzi wa NATO kuelekea mipaka ya Russia.
Kwa sasa, Russia inaongoza duniani kwa kuwa taifa lililowekewa vikwazo vingi zaidi, ikizipita hata Iran, Venezuela, Myanmar, na Cuba.