Waandishi Wahispania wataka kuhitimishwa vita Gaza
(last modified Fri, 06 Jun 2025 02:29:43 GMT )
Jun 06, 2025 02:29 UTC
  • Waandishi Wahispania wataka kuhitimishwa vita Gaza

Waandishi zaidi ya 400 wa Uhispania wamesema kuwa, utawala wa Israel umekiuka sheria za kimataifa na wametoa mwito wa kusitishwa mara moja mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Gaza.

Waandishi hawa wanaofanya kazi katika nyanja za fasihi ya watoto, vijana na watu wazima wamesema katika taarifa yao ya pamoja: "Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa kufanya kazi kukomesha mara moja mashambulizi haya ya kiholela na kukomesha biashara ya zana za kijeshi zinazotumiwa dhidi ya raia."

Waandishi hao wameutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ukiukaji wa "mara kwa mara" wa sheria za kimataifa na kusisitiza kwamba, Israel inapaswa kuwajibishwa kwa mauaji ya raia na kwamba ni lazima kuchukuliwa hatua ili kuhakikisha kwamba "vitendo hivyo vya kikatili" kamwe havirudiwi tena popote duniani.

Waandishi hao wa Uhispania wamesema: "Mambo haya hayana uhalali wowote. Watoto si wapiganaji. Huu sio ulimwengu tuliouwazia. Huu sio ulimwengu tulioutaka."

Hayo yanajiri siku chache baada ya Baraza la Jiji la Barcelona nchini Uhispania kutangaza kuvunja uhusiano wa kitaasisi na utawala wa Israel kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Ijumaa iliyopita baraza hilo lilipiga kura ya kuvunja uhusiano wa kitaasisi na utawala wa Israel na kusitisha makubaliano yake ya urafiki na Tel Aviv "hadi sheria ya kimataifa itakapoheshimiwa na kuhakikishiwa haki za kimsingi za watu wa Palestina."

Aidha haya yanajiri siku chache baada ya Jose Manuel Albares, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania kusema kuwa, nchi yake haina nia ya kutoa nasaha kwa yeyote; lakini njia pekee ya kupata amani ni kuitambua nchi ya Palestina, kwani ndiyo njia pekee ya kupatikana amani.