Ufaransa yasisitiza kuhusu azma ya kutambua taifa la Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, amesema kuwa Paris bado imejizatiti kutambua rasmi taifa la Palestina katika mkutano wa Umoja wa Mataifa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza na kituo cha redio cha RTL cha Ufaransa, Barrot alipoulizwa iwapo Ufaransa, ambayo itakuwa mwenyeji mwenza wa mkutano huo na Saudi Arabia, iko tayari kuchukua hatua ya kuitambua Palestina kama taifa huru, amesisitiza: “Tumejizatiti kufanya hivyo.”
Waziri huyo amesema kuwa Ufaransa na Saudi Arabia zitaweka wazi dhamira yao ya kuondoa vikwazo vilivyopo katika kutambuliwa kwa taifa la Palestina katika mkutano huo wa kimataifa utakaoandaliwa kati ya tarehe 17 hadi 20 Juni mjini New York.
Barrot amesema: “Ufaransa ingeweza kuchukua hatua ya kinembo. Lakini huo si mwelekeo tuliochagua, kwa sababu tuna wajibu maalum, sisi ni Ufaransa, mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."
Ameongeza kuwa lengo la Ufaransa si tu kutoa tamko bali kubadilisha hali halisi ya kisiasa, na kuhakikisha kuwa taifa la Palestina linakuwa halali, linaaminika na linawezekana katika mtazamo wa kimataifa.
Ufaransa inawaongoza washirika wake barani Ulaya, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Uholanzi, na Ubelgiji, katika kushinikiza kutambuliwa kwa Palestina kwa pamoja wakati wa mkutano huo muhimu.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anatumai kutumia jukwaa hili kufufua mazungumzo ya amani kati ya utawala wa Israel na Wapalestina, kupitia hatua ya mataifa ya Ulaya kutambua rasmi taifa la Palestina.
Ikiwa Ufaransa na Uingereza zitachukua hatua hii, zitakuwa mataifa ya kwanza ya kundi la G7 kutambua rasmi taifa la Palestina, jambo ambalo limekuwa mada kuu ya matakwa ya Wapalestina kwa miongo mingi.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, msemaji wa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Keir Starmer, alisema kuwa Uingereza iko tayari kushirikiana na washirika wake na mataifa ya kanda kusaidia ujenzi wa misingi ya taifa huru la Palestina.
Mpaka sasa, zaidi ya mataifa 140 wanachama wa Umoja wa Mataifa tayari yametambua taifa la Palestina, huku Hispania, Ireland, na Norway zikijiunga na orodha hiyo mwaka jana.