Upanga wa China uko juu ya viwanda vya kijeshi vya Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i127396-upanga_wa_china_uko_juu_ya_viwanda_vya_kijeshi_vya_magharibi
Vikwazo ambayo China imeziwekea nchi za Ulaya na Marekani katika usafirishaji wa madini adimu na sumaku zinazotengenezwa kutokana na madini hayo, vimeleta changamoto kubwa kwa shughuli za kijeshi za Marekani na washirika wake wa Ulaya.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jun 10, 2025 04:10 UTC
  • Upanga wa China uko juu ya viwanda vya kijeshi vya Magharibi

Vikwazo ambayo China imeziwekea nchi za Ulaya na Marekani katika usafirishaji wa madini adimu na sumaku zinazotengenezwa kutokana na madini hayo, vimeleta changamoto kubwa kwa shughuli za kijeshi za Marekani na washirika wake wa Ulaya.

Gazeti la New York Times liliripoti jana Jumatatu kwamba vikwazo vya China katika uuzaji wa madini adimu nje ya nchi vimehatarisha uwezo wa Marekani na Ulaya wa kuimarisha uzalishaji wa silaha za kisasa na za hali ya juu zilizopungua kutokana na vita vya Ukraine na Ghaza.

Moja ya madini hayo muhimu ambayo China imesimamisha kuziuzia nchi za Ulaya na Marekani, ni dutu inayoitwa "samarium."

Dutu hii ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa sumaku zinazokabiliana na joto. Sumaku hizo zinaweza kustahimili halijoto ya kiwango cha kuyeyusha risasi, na ni muhimu sana katika injini za umeme zinazokwenda kwa kasi ya hali ya juu ambazo hutumika katika maeneo yaliyozibwa kila sehemu, kama vile koni za makombora au ndege za kivita za F-35.

Kila ndege ya Lockheed Martin F-35 inahitaji takriban kilo 22.5 za sumaku za madini ya samarium. Stanley Trott, mtaalamu wa madini katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Denver Metropolitan ambaye pia ni mtaalamu wa sumaku za samarium tangu miaka ya 1970, ameliambia gazeti la The Washington Post kwamba tofauti na aina nyingine sita adimu za madini ya sumaku ambayo yanahitajika mno kwa matumizi ya kiraia,  aina hii ya madini ya samarium inatumika takriban kwa matumizi ya kijeshi tu.

China ina asilimia 90 ya uwezo wa ulimwengu wa kuchimba na kusafisha madini adimu na kuzalisha sumaku kwa kutumia madini hayo.

Kwa miaka mingi China imekuwa muuzaji pekee duniani wa samarium. Kukataa Beijingi kuziuzia nchi za Ulaya na Marekani madini na sumaku zinazotengenezwa kwa madini hayo kumeviletea changamoto kubwa viwanda vya silaha vya Marekani na Ulaya, nchi ambazo zimetumia silaha zao nyingi katika vita vya Ukraine na Ghaza.