Kulaaniwa chuki dhidi ya Uislamu katika bunge la California, Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12859-kulaaniwa_chuki_dhidi_ya_uislamu_katika_bunge_la_california_marekani
Bunge la Jimbo la California nchini Marekani limepasisha muswada wa kulaani vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu.
(last modified 2026-03-03T16:16:59+00:00 )
Aug 08, 2016 13:20 UTC
  • Kulaaniwa chuki dhidi ya Uislamu katika bunge la California, Marekani

Bunge la Jimbo la California nchini Marekani limepasisha muswada wa kulaani vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu.

Bunge hilo sanjari na kushukuru ushiriki mkubwa wa Waislamu katika shughuli mbalimbali za maendeleo jimboni hapo na katika maeneo mengine ya nchi hiyo, Jumapili ya jana lilipasisha muswada ambao uliutaja mwezi huu wa Agosti kuwa mwezi wa kuwashukuru  Waislamu na kuizindua jamii. Muswada huo uliowasilishwa na Bill Quirk, mmoja wa wanachama wa hilo, ulipasishwa baada ya kuungwa mkono kwa asilimia kubwa na wajumbe wa vyama viwili vya Democratic na Republican. Wawakilishi wa bunge hilo la California walisema kwamba muswada huo ulikuwa na umuhimu wa kupasishwa kwa ajili ya kutambua, kuunga mkono, na kuarifisha nafasi muhimu ya Waislamu wa jimboni hapo na maeneo yote ya Marekani, sanjari na kuwaheshimu watu wa jamii hiyo sawa na raia wengine wa Marekani. Kwa mujibu wa Bill Quirk, matamshi yanayotolewa katika kampeni za uchaguzi wa rais mwaka huu nchini Marekani, yamelipelekea suala hilo kuwa na umuhimu mkubwa kuliko wakati mwingine wowote.

Baadhi ya maandishi ya chuki dhidi ya Uislamu kwenye kuta za msikiti

Muswada uliopasishwa pia, unalaani vitendo vya kibaguzi dhidi ya Waislamu vilivyoshika kasi baada ya shambulio la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001 nchini humo. Waandaaji wa muswada huo wamesema kuwa, jimbo la California lina zaidi ya misikiti 240, idadi ambayo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na ya misikiti katika majimbo mengine ya nchi hiyo na kwamba suala hilo linabainisha ni kwa kiasi gani jimbo hilo linawapa umuhimu Waislamu. Rasimu ya muswada wa kuutangaza mwezi huu wa Agosti kuwa mwezi wa 'Kufahamu na kuwashukuru Waislamu' iliwasilishwa pia wiki iliyopita na Bill Quirk kwa lengo la kuchunguzwa  na wawakilishi wa Congress ya Marekani. Hii sio mara ya kwanza kwa viongozi wa majimbo kadhaa ya Marekani kutambua nafasi chanya ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo. Mwaka 2014 baraza la mji wa Los Angeles, liliutaja mwezi wa Julai kama 'Mwezi wa Turathi za Kiislamu.'  Gazeti la The Huffington Post limetoa ripoti kuhusiana na matukio yanayohusiana na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu kwa kuandika kuwa, mwaka huu pekee karibu matukio 233 yalisajiliwa ambapo matatu kati ya hayo yalitokea mwezi jana katika jimbo la California.

Wenye chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani

Moja ya kesi hizo za chuki dhidi ya Uislamu ni kushambuliwa na kuvunjiwa heshima mwanamke wa Kiislamu aliyekuwa amevalia vazi la stara la hijabu wakati alipokuwa katika moja ya maduka makubwa ya mji wa San Leandro jimboni hapo. Ripoti zilizotolewa kutoka baraza la uhusiano wa Kiislamu jimboni hapo inaelezea ongezeko la asilimia 58 la mashambulizi ya kibaguzi dhidi ya jamii ya Waislamu kati ya mwaka 2014-2015, ambapo inaarifiwa kuwa vitendo hivyo vinachangiwa na baadhi ya matamshi ya wagombea katika kukaribia uchaguzi wa rais baadaye mwaka huu. Alaa kulli hal, hatua ya kulaaniwa vitendo vya chuki dhidi ya dini ya Kiislamu katika bunge la jimbo la California nchini Marekani, inabainisha umuhimu wa jamii ya wafuasi wa dini hii tukufu nchini humo.