Wabunge wa Ulaya watoa wito wa kuwekewa vikwazo Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128720
Wabunge 60 wa Bunge la Ulaya wametia saini barua ya pamoja wakitaka hatua za haraka zichukuliwe kuwaokoa raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-07-26T11:21:05+00:00 )
Jul 25, 2025 02:43 UTC
  • Wabunge wa Ulaya watoa wito wa kuwekewa vikwazo Israel

Wabunge 60 wa Bunge la Ulaya wametia saini barua ya pamoja wakitaka hatua za haraka zichukuliwe kuwaokoa raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Barua hiyo inasema: "Watoto wa Gaza wanakufa kwa njaa, wakati mwitikio wa Umoja wa Ulaya umekuwa mdogo kwa maneno dhaifu na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kukomesha maafa haya."

Wawakilishi hao wametaka kuitishwe kikao cha dharura cha Baraza la Mashauri ya Kigeni la Umoja wa Ulaya ili kufikiria kuchukua hatua dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel.

Katika barua yao hiyo, Wabunge wa Bunge la Ulaya wamesisitiza kwamba tunataka kifurushi cha vikwazo dhidi ya utawala wa kizayuni kiwasilishwe kwa ajili ya kuidhinishwa na Baraza la Mashauri ya Kigeni la Umoja wa Ulaya.

Katika upande mwingine, Kaja Kallas, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, amedai kuwa “mauaji ya raia wasio na hatia wa Kipalestina lazima yakome,” la sivyo, “Machaguo Yote Yatazingatiwa dhidi ya Israel.”

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Kallas amelaani mauaji ya watu wasio na ulinzi Gaza na kusema, "Kuuawa kwa raia wanaotafuta msaada huko Gaza hakufai kutetewa kwa njia yoyote ile.” Ameongeza kuwa anaendelea kufanya mazungumzo na mashirika ya kimataifa ili kusaidia kufikisha misaada haraka Gaza, huku akisisitiza kuwa kushambulia vituo vya misaada ni kitendo kinachostahili kulaaniwa vikali.

Ikumbukwe kuwa, kwenye kikao cha tarehe 15 Julai mjini Brussels, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walijadili uwezekano wa kusimamisha mkataba wa ushirikiano na Israel na hata kuiwekea vikwazo, lakini hakuna hatua yoyote iliyoafikiwa: Si vikwazo vya silaha, si kusitisha mikataba ya biashara wala hata masharti ya viza.