Ubelgiji nayo kuitambua rasmi Palestina, yaamua kuiwekea Israel vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130304-ubelgiji_nayo_kuitambua_rasmi_palestina_yaamua_kuiwekea_israel_vikwazo
Ubelgiji imetangaza kuwa itatambua rasmi taifa la Palestina kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) baadaye mwezi huu. Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prevot.
(last modified 2025-09-01T23:29:29+00:00 )
Sep 01, 2025 23:29 UTC
  • Maxime Prevot
    Maxime Prevot

Ubelgiji imetangaza kuwa itatambua rasmi taifa la Palestina kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) baadaye mwezi huu. Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prevot.

"Palestina itatambuliwa na Ubelgiji katika kikao cha Umoja wa Mataifa! Na vikwazo vikali vitawekwa dhidi ya serikali ya Israel," Prevot, ambaye pia ni naibu waziri mkuu, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X mapema leo Jumanne.

Prevot amesema Ubelgiji pia itaweka "vikwazo vikali" 12 kwa Israel, pamoja na kupiga marufuku kuagiza bidhaa kutoka kwenye vitongoji vya walozi wa kizayuni, na vilevile "kupitia sera za ununuzi wa umma na kampuni za Israel".

Ameongeza kuwa tangazo hilo limetolewa "kwa kuzingatia maafa ya binadamu yanayotokea Palestina, haswa huko Gaza".

Gaza

Mwishoni mwa mwezi Julai, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitangaza kuwa nchi yake itaitambua rasmi Palestina katika mkutano wa UNGA, utakaofanyika kuanzia Septemba 9 hadi 23 mjini New York.

Kufuatia hatua hiyo, nchi nyingine kadhaa zimetangaza kufanya hivyo, ingawa baadhi zimesema zinakusudia kuweka masharti kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu, nchi 147, zinazowakilisha asilimia 75 ya wanachama wa Umoja wa Mataifa, tayari zimelitambua rasmi taifa la Palestina.

Tangazo la Ubelgiji linakuja wakati vita vya Israel dhidi ya Gaza vimeua watu 63,459 na kujeruhi wengine 160,256.

Mwezi Julai mwaka huu pia, waendesha mashtaka wa Ubelgiji waliwasilisha mashtaka ya uhalifu wa kivita dhidi ya wanajeshi wawili wa Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kufuatia madai kwamba walishiriki katika ukatili dhidi ya Wapalestina huko Gaza.