WHO: Kujiua husababisha kifo kimoja kati ya 100 duniani
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, zaidi ya kifo kimoja kati ya kila vifo 100 duniani husababishwa na kujitoa uhai. Shgirika hilo limetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kukabiliana na dharura ya afya ya akili, hasa miongoni mwa vijana.
Taarifa ya WHO imesema kuwa, ingawa kiwango cha watu wanaojitoa uhai duniani kimepungua kwa kiasi fulani katika miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na miaka ya nyuma, lakinii kasi ya kupambana na tatizo hili bado ni ndogo mno.
Mwaka 2021 — ambao ndio mwaka wa mwisho wenye takwimu kamili — unaonyesha kuwa, kulikuwa na makadirio ya watu 727,000 waliokufa kwa kujiua kote duniani, kwa mujibu wa shirika hilo la afya duniani.
Devora Kestel, Kaimu Mkuu wa idara ya magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili karika Shitrika la Afya Duniani (WHO) amesema, "duniani kote, kujitoa uhai kunachangia zaidi ya kifo kimoja kati ya vifo 100, na kwa kila kifo kimoja, kuna majaribio ya kujitoa uhai mara 20,”.
Vifo hivyo "vimeathiri maisha na riziki za mamilioni ya watu, kwani marafiki, walezi na wapendwa wamelazimika kukabiliana na maumivu yasiyoelezeka,” aliongeza kuwaambia waandishi wa habari.
Ripoti ya WHO iitwayo World Mental Health Today imeonyesha kuwa kujitoa uhai bado ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo miongoni mwa vijana bila kujali maeneo na hali zao za kiuchumi.
Mwaka 2021, kujitoa uhai kilikuwa chanzo cha pili cha vifo kwa wasichana na wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 29, na chanzo cha tatu cha vifo kwa wavulana wa umri huohuo.