"Vikwazo vya Marekani, Ulaya vimeua watu milioni 38 tangu 1970"
Tahariri iliyoandikwa na tovuti ya habari ya kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar imekosoa muenendo wa nchi za Magharibi kutumia vikwazo kuziadhabu nchi zinazozitazama kama maadui; ikieleza kuwa, vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya vimeua watu zaidi ya milioni 38 kote duniani tangu 1970.
Marekani na Ulaya kwa muda mrefu zimetumia vikwazo vya upande mmoja kama chombo cha ubabe, kutia adabu na hata kusambaratisha serikali za eneo la kusini mwa dunia, ambazo zinataka kuondosha ushawishi wa Magharibi, kuandaa njia huru, na kuanzisha mifumo ya mamlaka ya kujitawala.
Uchambuzi huo wa kisiasa umenukuu utafiti mpya uliochapishwa mwaka huu katika jarida la The Lancet Global Health, ambao ulitoa mtazamo wa kimataifa kwa mara ya kwanza. Ukiongozwa na mchumi Francisco Rodriguez katika Chuo Kikuu cha Denver, utafiti huo ulihesabu jumla ya vifo vilivyozidi vilivyohusishwa na vikwazo vya kimataifa kutoka 1970 hadi 2021.
Matokeo ya utafiti huo ni ya kushangaza. Katika makadirio yao ya kati, watafiti waliona kuwa vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na Marekani na EU tangu 1970 vinahusishwa na vifo milioni 38.
Katika baadhi ya miaka, katika miaka ya 1990, zaidi ya watu milioni moja waliuawa. Mnamo 2021, mwaka wa hivi karibuni wa data, vikwazo vilisababisha vifo zaidi ya 800,000.
Hivi karibuni, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Abbas Araghchi alisisitiza kuwa: "Wakati umefika kwa vikwazo visivyo vya kibinadamu vilivyowekwa na Marekani na washirika wake kutambuliwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu."
Katika miaka ya 1970, kwa wastani, takriban nchi 15 duniani zilikuwa chini ya vikwazo vya upande mmoja vya Magharibi katika mwaka wowote.