WHO: Mpox sio dharura tena ya afya ya kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130494-who_mpox_sio_dharura_tena_ya_afya_ya_kimataifa
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, ugonjwa wa Mpox hauzingatiwi tena kuwa dharura ya afya ya kimataifa.
(last modified 2025-09-06T22:52:55+00:00 )
Sep 06, 2025 22:52 UTC
  • WHO: Mpox sio dharura tena ya afya ya kimataifa

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, ugonjwa wa Mpox hauzingatiwi tena kuwa dharura ya afya ya kimataifa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye amebainisha kwamba uamuzi huo umezingatia ushauri wa Kamati ya Dharura ya WHO, ambayo hukutana kila baada ya miezi mitatu kutathmini hali ya mripuko.

Amesisitiza kuwa ingawa hali ya dharura imeondolewa, lakini hali hiyo haimaanishi kuwa tishio la Mpox limekwisha kabisa na kwamba, juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zimesitishwa.

Shirika la Afya Duniani limesema katika taarifa yake hiyo kwamba,  hatua hiyo ni ishara ya mafanikio ya juhudi za kimataifa za kudhibiti ugonjwa huo, lakini pia ni wito wa kuendelea kuwa waangalifu na kuimarisha mifumo ya afya ili kuzuia miripuko ya baadaye.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) ugonjwa wa Mpox ambao umeenea katika nchi za Kiafrika na kuua mamia ya watu, bado ni dharura ya kiafya katika bara hilo.

Mapitio yaliyofanywa na Kundi la Ushauri wa Dharura yanaonyesha kuwa hali ya mambo inaashiria kuwa kulikuwa na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Mpox katika nchi kama Ghana, Liberia, Kenya, Zambia na Tanzania.

Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi, ambao hapo awali ulijulikana kwa jina la ugonjwa wa tumbili, kabla ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kubadili jina lake mwaka wa 2022 kutokana na malalamiko kwamba jina hilo linaibua hisia za ubaguzi na unyanyapaaji.