Jinsi Google ilisvyoshirikiana na Israel kuficha njaa huko Gaza, Palestina
Katika jaribio la kuficha njaa ya kimfumo ambayo imesababishwa na Israel huko Gaza, serikali ya Tel Aviv imetia saini mikataba mikubwa ya utangazaji na kampuni za kimataifa kama vile Google, X, na zingine kusambaza propaganda zinazokana uwepo wa njaa katika Ukanda wa Gaza.
Ripoti ya uchunguzi ya Drop Site News imefichua kuwa, Israel ilitia saini mkataba wa dola milioni 45 na kampuni ya Google ili kuficha dalili za njaa huko Gaza, sanjari na kuongezeka kwa maonyo ya kimataifa kuhusu matokeo mabaya ya kuendelea kuwatesa Wapalestina kwa njaa.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotayarishwa na Abdel Qader Arada, juhudi hizi zinaangazia jinsi serikali ya Benjamin Netanyahu- ambaye anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu- inavyotumia propaganda na vyombo vya habari kama silaha katika vita vya Gaza.
Drop Site News inasema: Mkataba wa miezi sita ulitiwa saini moja kwa moja kati ya Google na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na kwa mujibu wa uchunguzi huo, lengo lake kuu lilikuwa kuficha njaa ya makusudi inayoangamiza watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Kupitia makubaliano hayo, kampuni ya Google ilichapisha tangazo linaloonyesha watu wakitayarisha chakula katika Ukanda wa Gaza. Video hiyo iliandamana na maandishi: "Kuna chakula huko Gaza, na mengine yasemwayo ni uwongo."
Kampeni hiyo haikuishia kwa kampuni ya Google, bali ilipanuliwa na kujumuisha watu wenye ushawishi wa Marekani, pamoja na matumizi makubwa ya pesa kwa ajili ya kufadhili matangazo yaliyosambazwa kupitia Google, YouTube, X, Meta, na majukwaa mengine ya kimagharibi.
Uchunguzi wa Drop Site News pia unafichua kuwa, serikali ya Israel ilitumia dola milioni 3 kwa kandarasi nyingine ya utangazaji kwenye jukwaa la X, na pia iliilipa kampuni ya utangazaji ya Ufaransa na Israel Outbrain Tides takriban dola milioni 2.1 kwa ajili ya matangazo ya propaganda za kupotosha ukweli na kuonyesha kuwa hakuna njaa katika Ukanda wa Gaza.
Uchunguzi huo umeashiria ukosoaji wa Mtaalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa, Francesca Albanese kwa kandarasi ya Project Nimbus iliyotiwa saini na Google na Amazon mwaka 2021 ili kutoa huduma za kompyuta ya wingu kwa serikali na jeshi la Israel.
Albanese anasema Google inafaidika kutokana na "mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza."
Hadi sasa mamia ya raia wa Palestina wamefariki dunia kwa njaa ya makusudi katika Ukanda wa Gaza.