Hasira yatanda Uingereza kuhusu ziara ijayo ya Herzog: Wanasiasa wataka akamatwe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130516-hasira_yatanda_uingereza_kuhusu_ziara_ijayo_ya_herzog_wanasiasa_wataka_akamatwe
Ziara iliyopangwa kufanywa wiki ijayo na Rais wa Israel, Isaac Herzog, nchini Uingereza imezusha wimbi la upinzani na hasira katika ya duru za kisiasa, huku kukitolewa wito wa kususiwa na hata kusitishwa safari hiyo katika kipindi cha sasa ambapo utawala wa Israel unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. .
(last modified 2025-09-07T08:28:18+00:00 )
Sep 07, 2025 08:28 UTC
  • Hasira yatanda Uingereza kuhusu ziara ijayo ya Herzog: Wanasiasa wataka akamatwe

Ziara iliyopangwa kufanywa wiki ijayo na Rais wa Israel, Isaac Herzog, nchini Uingereza imezusha wimbi la upinzani na hasira katika ya duru za kisiasa, huku kukitolewa wito wa kususiwa na hata kusitishwa safari hiyo katika kipindi cha sasa ambapo utawala wa Israel unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. .

Katika muktadha huo, wabunge wa Uingereza wametoa wito kwa mawaziri wa serikali kutompokea na kumsusia Rais huyo wa Israel kutokana na mashambulizi makubwa ya kijeshi yanayofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Sky News inasema, ingawa Isaac Herzog, ambaye ni kutoka chama tofauti cha kisiasa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hakabiliwi na hati ya kimataifa ya kukamatwa, lakini kutajwa tu ziara yake nchini Uingereza kumezua maandamano na upinzani mkubwa.

Mbunge wa chama cha Labour, Sarah Champion, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Teule ya Maendeleo ya Kimataifa, amesema kukutana na Herzog "kutadhoofisha" nia ya serikali ya kuilaani Israel kutokana na vitendo vyake katika Ukanda wa Gaza, na kuongeza: "Uingereza imetambua tishio la kweli la mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel, hivyo ni ujumbe gani tunatuma ikiwa mkutano huu sio wa amani?"

Kwa upande wake, waziri kivuli wa zamani wa fedha wa chama cha Labour, John McDonnell amesema ziara hiyo "itasababisha aibu kwa Uingereza."

Mbunge Zara Sultana, ambaye amejiuzulu kutoka chama cha Labour ili kuongoza chama kipya na Jeremy Corbyn, ameleza kukasirishwa sana na ziara hiyo na kutoa wito wa kukamatwa kwa Rais wa Isarel, Isaac Herzog.

Zara Sultana

Wakati huo huo, polisi wa mji mkuu wa Uingereza walitangaza jana Jumamosi kwamba idadi ya waliokamatwa katika maandamano ya waungaji mkono kwa Wapalestina mjini London imezidi watu 425.

Polisi imeeleza kuwa wengi wamekamatwa kwa madai ya kuunga mkono shirika lililopigwa marufuku la Palestine Action.