Uhispania kuiwekea Israel vikwazo kamili vya silaha
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130532-uhispania_kuiwekea_israel_vikwazo_kamili_vya_silaha
Serikali ya Uhispania imetangaza kuwa, inapanga kuiwekea Israel vikwazo kamili vya silaha kutokana na jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-09-07T23:02:31+00:00 )
Sep 07, 2025 23:02 UTC
  • Uhispania kuiwekea Israel vikwazo kamili vya silaha

Serikali ya Uhispania imetangaza kuwa, inapanga kuiwekea Israel vikwazo kamili vya silaha kutokana na jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu katika Ukanda wa Gaza.

Kesho Jumanne Uhispania inatazamiwa kupiga kura juu ya dikrii ya kifalme ya kuweka vikwazo kamili vya silaha dhidi ya Israel.

 Hatua hiyo itapiga marufuku shughuli zote za kijeshi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na inaweza kumtangaza Waziri Mkuu Netanyahu na mawaziri muhimu wa utawala huo kuwa watu wasiostahili.

Hatua hiyo inaashiria kuongezeka migawanyiko ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na namna ya kuamiliana na kushirikiana na Israel.

Uhispania imekuwa ikikosoa sera za Israeli huko Gaza na Ukingo wa Magharibi. Waziri Mkuu Pedro Sánchez hivi majuzi aliita Israel "jimbo la mauaji ya kimbari" bungeni. Waziri wa Mambo ya Nje José Manuel Albares alisema Uhispania itashinikiza Umoja wa Ulaya kusitisha makubaliano yake ya ushirikiano na Israel na kuunga mkono vikwazo vya silaha katika umoja huo.

Hivi majuzi Yolanda Diaz Naibu Waziri Mkuu wa Pili wa Uhispania na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Kijamii alibainisha kwamba, kuna ulazima wa kusitishwa mikataba yote na kusimamisha biashara na utawala wa Kizayuni ili kukabiliana na "uchumi wa mauaji ya kimbari."

Wakati huo huo, Waziri wa Mashauuri ya Kigeni wa Uhispania ameunga mkono wito wa kuondolewa timu ya waendesha baiskeli ya Israel kwenye mashindano ya mchezo huo yanayoendelea, kufuatia maandamano na malalamiko ya waungaji mkono wa Palestina nchini humo.