Uhispania kupiga marufuku meli na ndege zinazobeba silaha za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130582-uhispania_kupiga_marufuku_meli_na_ndege_zinazobeba_silaha_za_israel
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, ametangaza hatua mpya kali za kidiplomasia na kiusalama zenye lengo la kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili usitishe mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 08, 2025 23:51 UTC
  • Pedro Sanchez
    Pedro Sanchez

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, ametangaza hatua mpya kali za kidiplomasia na kiusalama zenye lengo la kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili usitishe mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Akizungumza jana Jumatatu, Sanchez alisema kuwa serikali ya Madrid itapiga marufuku meli na ndege zinazobeba silaha au mafuta kwa ajili ya Israel kuingia katika anga ya Hispania au kutia nanga katika bandari zake.

Madrid pia imeahidi kuongeza msaada kwa Mamlaka ya Palestina na Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kwa kiasi cha euro milioni 10, pamoja na euro milioni 150 za ziada kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa Gaza ifikapo mwaka 2026.

Aidha, Uhispania itapiga marufuku bidhaa zinazotengenezwa katika makazi ya walowezi wa Kiyahudi ndani ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Katika hotuba yake kwa umma, Sanchez amesema kuwa hatua hizi zinalenga “kusitisha mauaji ya kimbari huko Gaza, kuwawajibisha wahusika na kuwaunga mkono raia wa Palestina.”

Sanchez amesisitiza: "Israel haijilindi, bali inaangamiza watu wasio na ulinzi." Ameongeza kuwa anatumaini hatua hizo zitamshinikiza Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kupunguza mateso yanayowakumba Wapalestina.

"Tunajua hatua hizi hazitoshi kusitisha uhalifu wa kivita, lakini tunatumaini zitasaidia kuzidisha shinikizo na kupunguza mateso ya watu wa Palestina."

Sanchez ameonya kuwa Uhispania itapiga marufuku kuingia nchini kwa mtu yeyote aliyeshiriki moja kwa moja katika mauaji ya kimbari ya Gaza.

Amesisitiza kuwa ingawa Uhispania haiwezi kusitisha vita peke yake, “hilo halina maana kwamba hatuwezi kujaribu.”

Marekani imetajwa kuwa msambazaji mkuu wa misaada ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja kwa Israel, ikiwemo fedha, silaha, risasi na misaada ya kidiplomasia.

Balozi wa Marekani katika utawala wa Israel ameripotiwa kuhalalisha mauaji ya Gaza kama “vita takatifu dhidi ya Waislamu,” akifananisha mzozo huo na mapambano ya kiroho ya “mbingu dhidi ya jahanamu,” kwa kutumia lugha inayokumbusha zama za Vita vya Msalaba.

Tangu Tel Aviv ilipoanzisha mashambulizi mnamo Oktoba 2023, takriban Wapalestina 64,400, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameripotiwa kuuawa.

Waziri mkuu wa Israel Netanyahu, anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa kuhusika na mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita, anadai kuwa anapambana na magaidi.