Marekani ina ndoto gani kuhusu mafuta ya Venezuela?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135292-marekani_ina_ndoto_gani_kuhusu_mafuta_ya_venezuela
Kufuatia operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela, swali muhimu limeibuka: Washington ina mipango gani kwa ajili ya mafuta ya nchi hiyo?
(last modified 2026-01-09T14:22:17+00:00 )
Jan 09, 2026 14:22 UTC
  • Marekani ina ndoto gani kuhusu mafuta ya Venezuela?

Kufuatia operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela, swali muhimu limeibuka: Washington ina mipango gani kwa ajili ya mafuta ya nchi hiyo?

Baada ya kuvamia Venezuela na kumteka nyara Rais halali wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kwamba Caracas itauza mafuta yenye thamani ya dola bilioni 2 kwa Washington, hatua ambayo itabadilisha njia ya mafuta ya Venezuela badala ya China. Awali Trump alisema amemtaka rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez, aipe Marekani na makampuni binafsi ya nchi hiyo "uwezo kamili" wa kuingia katika sekta ya mafuta nchini humo.

Jumanne iliyopita Trump aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya mitandao ya kijamii, Truth Social akisema: "Ninafurahi kutangaza kwamba mamlaka ya mpito nchini Venezuela imekubali kutuma Marekani kati ya mapipa milioni 30 na 50 ya mafuta yenye ubora." Trump aliongeza: "Mafuta yatakayotumwa na Venezuela nchini Marekani yatauzwa kwa bei ya soko." Rais wa Marekani pia alisema kwamba udhibiti wa mapato utakuwa mikononi mwake kama Rais wa Marekani, akidai: "Nitasimamia na kuhakikisha kwamba pesa hizi zinatumika kwa manufaa ya watu wa Venezuela na Marekani." Trump alimalizia kwa kueleza kwamba amemtaka Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright kutekeleza mpango huo mara moja, akisema: "Shehena hiyo itasafirishwa na meli za mafuta moja kwa moja hadi kwenye gati za kupakua mizigo nchini Marekani."

Marekani inataka kudhibiti sekta ya mafuta ya Venezuela

Wakati huo huo chanzo kimoja chenye uhusiano na sekta ya mafuta ya Marekani kimesema: "Trump anataka hili lifanyike haraka iwezekanavyo ili aweze kulifanya lionekane kama ushindi mkubwa." 

Nukta muhimu zaidi ni kwamba, kupelekwa mafuta ya Venezuela huko Marekani kutalazimu kubadilisha njia ya usafirishaji wa bidhaa hiyo ambayo awali ilikuwa ikielekea China, kwani Beijing imekuwa mnunuzi mkubwa wa mafuta ya nchi hiyo katika muongo mmoja uliopita, hasa baada ya Marekani kuweka vikwazo kwa makampuni ya mafuta ya Venezuela mwaka wa 2020. Wakati huo huo, ongezeko la mauzo ya nje ya mafuta ya Venezuela kwa Marekani linaweza kuathiri makampuni ya Canada yanayouza mafuta mazito, na viwanda vidogo vya kusafisha mafuta vya China ambavyo vimekuwa vikitumia mafuta ya bei nafuu ya Venezuela katika miaka ya hivi karibuni na vimebadilishwa kwa ajili kusafisha aina hiyo ya mafuta. Hivyo basi, iwapo mafuta ghafi ya Venezuela yataelekezwa Marekani, viwanda hivyo vya kusafisha mafuta vitakabiliwa na gharama kubwa zaidi.

Venezuela ina mamilioni ya mapipa ya mafuta kwenye maghala ya kuhifadhia bidhaa hiyo ambayo haijaweza kuyauza nje kutokana na mzingiro na vikwazo vya Trump vya mwezi uliopita. Marufuku hiyo ilikuwa sehemu ya mpango wa Marekani wa kuishinikiza serikali ya Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, ambao hatimaye umeishia kwenye uvamizi wa kijeshi na kutekwa nyara Maduuro na mkewe.

Kama ripoti hiyo ni kweli, basi makubaliano hayo ya mafuta yanaonyesha kwamba Caracas imefungua viwanda vyake vya kusafisha mafuta kwa makampuni ya Marekani ili kuzuia uharibifu mkubwa zaidi na uingiliaji kati wa kijeshi na Washington. Hata hivyo maafisa wa serikali ya Venezuela na kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, Petróleos de Venezuela, bado hawajatoa maoni kuhusu madai ya Trump.

Tangazo la utawala wa Trump kwamba mafuta ya Venezuela sasa yatapelekwa Marekani baada ya operesheni ya kijeshi na kutekwa nyara Nicolas Maduro na mkewe, linatambuliwa kuwa ni hatua nyeti katika sera ya nishati ya Marekani na siasa za kijeopolitiki. Hatua hii inaonyesha kwamba Washington haikusudii  mabadiliko ya kisiasa pekee huko Caracas, bali lengo lake kuu ni kudhibiti rasilimali kubwa ya mafuta ya Venezuela na kuirudisha kwenye mzunguko wa uchumi wa Magharibi.

Malengo ya utawala wa Trump yanaweza kuchunguzwa katika ngazi kadhaa. Kwanza, kuhakikisha usalama wa nishati wa Marekani katika hali ambapo soko la mafuta duniani linakabiliwa na mabadiliko makubwa. Venezuela, ikiwa na akiba kubwa zaidi ya mafuta iliyothibitishwa duniani, inaweza kuwa chanzo cha kuaminika cha kupunguza utegemezi wa Marekani kwa mafuta ya Asia Magharibi na kushindana na wazalishaji wa OPEC.

Pili, ni kurejesha makampuni ya mafuta ya Marekani kwenye biashara ya uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ya Venezuela. Miundombinu ya mafuta ya nchi hiyo imeharibiwa na vikwazo vya miaka mingi na mgogoro wa kiuchumi, na Washington inakusudia kuchukua udhibiti wa biashara ya uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ya nchi hiyo ya Amerika Kusini kwa kuwekeza katika makampuni yake makubwa ya mafuta.

Tatu, ni kutumia mafuta kama chombo cha mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi dhidi ya wapinzani wa kimataifa, hasa China na Russia, ambazo zimekuwa washirika wakuu wa nishati wa Venezuela katika miaka ya hivi karibuni.

Athari ya sera hii kwenye uhusiano wa mafuta wa Venezuela na China na nchi zingine itakuwa kubwa. Katika miaka ya hivi karibuni China imewekeza mabilioni ya dola katika tasnia ya mafuta ya Venezuela na inapokea sehemu kubwa ya mafuta ya nchi hiyo chini ya mikataba ya muda mrefu. Kuingia Marekani katika uwanja huo na udhibiti wa mauzo ya nje ya mafuta ya Venezuela kutabana uwezo wa China kufika kwenye rasilimali hizo na kunaweza kusababisha mvutano mkubwa kati ya Washington na Beijing. Russia, ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa kijeshi na nishati wa Caracas, pia itakabiliwa na kupungua kwa ushawishi wake nchini Venezuela. Mabadiliko haya, katika mlingano wa nguvu, yatazidisha ushindani wa kijiopolitiki na kisiasa katika Amerika Kusini na kufungua njia ya miungano mipya miongoni mwa mataifa makubwa.

Putin na Xi Jinping

Matukio haya pia yatakuwa na taathira mbaya za kiuchumi na kisiasa kwa nchi zingine, haswa wanachama wa OPEC na EU. Kuongezeka usafirishaji wa mafuta ya Venezuela kwenda Marekani kunaweza kuweka shinikizo kwa bei ya mafuta duniani na kudhoofisha nafasi ya baadhi ya wazalishaji wa jadi wa bidhaa hiyo. Ulaya, ambayo inatafuta vyanzo mbadala vya nishati, inaweza pia kukabiliwa na matatizo makubwa katika biashara zake na Venezuela.

Kwa ujumla, sera mpya ya utawala wa Trump kuhusu mafuta ya Venezuela inaonyesha mchanganyiko wa malengo ya kiuchumi, kijiopolitiki na kimkakati. Ingawa hatua hiyo inaweza kuimarisha usalama wa nishati na ushawishi wa Marekani katika masoko ya mafuta kwa muda mfupi, lakini kwa muda mrefu itazidisha hatari ya kuongeza ushindani na China na Russia kutokana na kuzuiwa nchi hizi mbili kuwepo nchini Venezuela, hasa katika sekta ya mafuta ya nchi hiyo, na vilevile kuzidisha mivutano ya kimataifa kutokana na kutoridhika kwa nchi za OPEC+ na sera ya mafuta ya Washington.