UN: Hali ya hatari Ethiopia inalenga wanadiplomasia na wanahabari
https://parstoday.ir/sw/news/world-i17656-un_hali_ya_hatari_ethiopia_inalenga_wanadiplomasia_na_wanahabari
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema anafuatilia kwa karibu matukio ya hivi sasa nchini Ethiopia na kueleza wasi wasi wake kuwa hali ya hatari iliyotangazwa hivi karibuni na serikali ya Addis Ababa, inawaathiri zaidi wanadiplomasia na waandishi wa habari.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2016 03:34 UTC
  • UN: Hali ya hatari Ethiopia inalenga wanadiplomasia na wanahabari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema anafuatilia kwa karibu matukio ya hivi sasa nchini Ethiopia na kueleza wasi wasi wake kuwa hali ya hatari iliyotangazwa hivi karibuni na serikali ya Addis Ababa, inawaathiri zaidi wanadiplomasia na waandishi wa habari.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa UN amesema kuna haja ya kufanyika mazungumzo ya amani yatakayozijumuisha pande zote za kisiasa, kijamii na kikaumu nchi humo, ili kuupatia ufumbuzi mzozo wa sasa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa UN

Siku chache zilizopita, Hairemariam Desalegn Waziri Mkuu wa Ethiopia alitangaza hali ya hatari kwa muda wa miezi sita nchini humo ili kurejesha amani baada ya machafuko ya wiki kadhaa yaliyosababisha raia kadhaa kuuawa na vile vile kuathiri viwanda na mashamba ya maua yanayomilikiwa na raia wengi wa kigeni.

Watu wasiopungua 55 waliuawa katika maandamano ya wapinzani wa serikali hivi karibuni, katika eneo la Oromia. Wapinzani wa serikali ya Addis Ababa wanasema watu zaidi ya 600 wameuawa katika machafuko ya miezi ya hivi karibuni nchini humo. 

Ghasia za hivi karibuni nchini Ethiopia

Maafisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch wameashiria hatua ya serikali ya Addis Ababa ya kupasisha sheria ya hali ya hatari kwa kipindi cha miezi sita nchini Ethiopia na uwezekano wa kuzidishwa utawala wa kijeshi na kipolisi katika maeneo ya mijini na kusema kuwa: Kutangazwa hali ya hatari si njia bora ya kusimamisha malalamiko ya wananchi na kwamba serikali ya Ethiopia inapaswa kutazama upya hatua hiyo.